Yanga kikitoka chuma, kinashuka chuma zaidi

Yanga wana msemo wao mmoja maridadi sana ‘Daima Mbele Nyuma Mwiko’, yaani hawana nafasi ya kujuta na wako tayari kuchukua maamuzi yoyote magumu na baada ya hapo hawaangalii nyuma.

Msemo wao huu kuna namna umekuwa ukiwaheshimisha katika misimamo yao katika mambo mbalimbali ndani ya klabu yao na kama hujajua wanamaanisha nini, cheki haya mambo sita hapa chini.

Anatoka Manji, GSM anaingia

Baada ya kuondoka Bilionea Yusuf Manji, Yanga ilikutana na kimbunga cha ukata mkubwa wa fedha kwa takribani misimu mitatu ila hawakukata tamaa. Walichangishana wanachama na mashabiki wao kuhakikisha mambo yanaenda.

Baada ya muda wakamshusha mkombozi mpya Bilionea mwingine Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ na sasa maisha yao yamekuwa mazuri na wanaendelea kutamba ukiwa ni msimu wa tatu sasa, wakionyesha ubabe ndani na nje ya uwanja.

Mabao ya Mayele vs Mabao ya Aziz KI

Msimu uliopita ulimalizika na kinara wa mabao alikuwa ni Fiston Mayele. Hakuna aliyeamini kama ataondoka Yanga na mwishowe ikawa hivyo.

Kwa sasa anakipiga Pyramids FC licha ya jitihada kubwa za kutaka abaki Jangwani. Ameibuka Mayele mwingine na anatupia anavyotaka. Ni Stephanie Aziz Ki na ndiye kinara wa mabao akiwa nayo 15 kwenye Ligi Kuu Bara na kipenzi cha mashabiki.

Anatoka Fei Toto, Pacome anaingia

Sakata lingine ambalo lilivuma zaidi msimu uliopita kwa Yanga ilikuwa ni kuondoka kwa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye alilazimisha na kufanikiwa kuondoka klabuni hapo na kwenda Azam.

Iliwaumiza sana mashabiki wa Yanga lakini ile ile ‘daima mbele nyuma mwiko’ ikashika nafasi akashushwa fundi mwingine Pacome Zouzoua ambaye balaa lake linaonekana na kila mtu anajua ni fundi wa namna gani.

Anatoka Nabi, Gamondi anaingia

Pigo lingine hili kwa Yanga hasa baada ya kutamba kwa miaka miwili ni pale aliyekuwa kocha wao Nasreddine Nabi kutangaza kuachana na klabu hiyo, baada ya Yanga kuwa na misimu miwili ya nguvu.

Timu pinzani nyingi zilichekelea zikiona kama ndio mwanzo wa kupotea kwa Yanga lakini tena akashushwa Mzungu wa kutoka America Kusini, Miguel Gamondi kutoka taifa la Argentina ambaye ni kama zaidi ya Nabi tu akaendeleza moto huo na sasa amebakiza pointi nane tu kuipa taji la kwanza timu hiyo.

Djuma anasumbua, Yao anashuka

Beki Mkongomani Djuma Shaban alisumbua sana Yanga msimu uliopita na ulipokwisha tu mabosi wa klabu hiyo wakakuna vichwa na kuingia msituni kutafuta nani atakuja kuzima kelele za beki huyo.

Ghafla, akashushwa kutoka Ivory Coast, Yao Akouassi akitokea ASEC Mimosas ya kwao na baada ya kuanza kazi tu haikuhitaji nguvu kubwa kwa mashabiki wa Yanga kumsahau ‘Sodaya ya Bemba’ tena akapotezwa kabisa na beki huyo mpya wa kazi.

Anaondoka Shikhalo, Diara anatua

Kuna msimu Yanga iliwashusha Metacha Mnata na Mkenya Farouk Shikhalo langoni.  Baada ya muda ikawapiga chini.

Ikaingia msituni tena na kumshusha Djigui Diarra na wakasahau kabisa changamoto za golini kwao kwani kipa huyo anavizia tuzo ya tatu ya kipa bora tangu atue nchini hakuna ambaye amempokonya tuzo hiyo, hawa jamaa kweli ni Daima mbele nyuma mwiko.

Related Posts