Dar es Salaam. Shirika la Tanzania Women Tapo, kwa kushirikiana na Hospitali ya Aga Khan Tanzania, linatarajia kuzindua kampeni ya afya kwa wanawake wachuuzi na wauzaji sokoni, mpango unaolenga kuwafikia takribani wanawake 31,000 katika mikoa yote 31 nchini.
Mpango huo uliopewa jina la ‘Msafara wa kitaifa wa wauzaji wanawake wa ndani wa Mama Samia’, unaolenga kutoa huduma ya afya na uwezeshaji wa kina kwa wafanyabiashara wanawake, unatarajiwa kuzinduliwa Desemba 10, 2024, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Women Tapo Tanzania, Lulu Nyapili amesema katika taarifa yake, kwamba mpango huo ulioandaliwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, unatoa mtazamo kamili wa kusaidia wanawake wajasiriamali na wachuuzi.
“Ni mkabala wa kina wa kusaidia uti wa mgongo wa wauzaji wanawake wa uchumi wetu wa ndani. Tunashughulikia afya, ustawi wa kiakili na uwezeshaji wa kiuchumi katika mpango mmoja wa kuleta mabadiliko,” ameelezea.
Nyapili amehimiza umma kushiriki katika matibabu ya bila malipo, kuhudhuria vipindi vya elimu ya afya na kusaidia wanawake wachuuzi wa eneo hilo katika jamii zao. Pia ametoa wito wa kuongeza ufahamu kuhusu mpango huo muhimu.
“Kila mwanamke wa masokoni ana umuhimu, kila mchuuzi ana hadithi, anastahili msaada, heshima na fursa ya kukua.
“Tunapojitayarisha kuzindua kampeni hii ya kitabibu ya kitaifa, hatusambazi huduma za matibabu tu. Tunasambaza matumaini, heshima, tunawekeza katika rasilimali ya nguvu zaidi ya taifa letu kwa wanawake wote,” amesisitiza.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Huduma za Afya ya Aga Khan, Sisawo Konteh, amesema ushirikiano kati ya taasisi hizo unalenga kutoa msaada wa matibabu kwa wanawake wa Tanzania.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ayoub Kibao, ambaye pia ni Mratibu wa Huduma za VVU mkoani humo, amesema Serikali inatambua mchango wa afya ya wanawake, kwani maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila afya ya wanawake.