Kambi, Muharami na wenzao wadai kuteswa wakati wakihojiwa.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini, Kambi Zuber Seif na wenzake wamedai kuteswa na kudhalilishwa utu wao na Maofisa wa Polisi kutoka Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini(DCEA), baada ya kukamatwa.

Kambi na wenzake watano, wanakabiliwa na  mashtaka nane yakiwemeo ya kuongoza genge na kusafirisha dawa za kulevya aina ya herone zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 43/2023 ni aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba, Muharami Sultani(40) maarufu kama Shilton; Maulid Mzungu(54) maarufu Mbonde, mkazi wa Kisemvule ambaye ni dalali wa viwanja na muuza nazi, ambaye pia ni kama yake mkubwa  na Muharami

Wengine ni Said Matwiko mkazi Magole; John Andrew maarufu Chipanda(40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph, ambaye ni mke wa Matwiko.

Kambi, kupitia wakili wake Dominicus Nkwera, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana Desemba 5, 2024, baada ya washtakiwa hao kumaliza kusomewa maelezo ya Mashahidi na Vielelezo( Commital Proceedings).

Washtakiwa hao walisomewa maelezo hayo na jopo la mawakili watatu wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisaidiana na Judith Kyamba na Roida Mwakamele.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kumaliza kusomewa Commital hiyo, Wakili Nkwera anatemtetea Kambi, aliwasilisha maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Kambi ambaye ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma Kigamboni, anadaiwa kukamatwa Horohoro na Maofisa wa DCEA, baada ya kupata taarifa kuwa anataka kutoroka nchini hivyo kuweka zuio katika mipaka ya Tanzania na katika viwanja vyote vya ndege, vilivyopo nchini.

Baada ya kukamatwa na kurudishwa Dar es Salaam, mshtakiwa huyo anadaiwa kuteswa na maofisa hao ili akiri tuhuma anakabiliwa nazo.

Wakili Nkwera alidai kuwa mteja wake (Kambi) alikamatwa Oktoba 31, 2022 na alivyokamatwa aliteswa na kudhalilishwa utu wake na maofisa hao.

“Mheshimiwa hakimu, naomba iingie katika kumbukumbu za mahakama, kuwa mteja wangu( Kambi) aliteswa sana na kudhalilishwa utu wake, nia na madhumuni wakitaka asaini maelezo ya onyo ambayo hakuyatoa na nyaraka ambazo alikutwa nazo,” alidai Wakili Nkwera na kuongeza.

Alidai mateso hayo yalipelekea Kambi asaini maelezo ambayo hakuyatoa.

“Hata alivyopelekwa kwa mlinzi wa amani kwa ajili ya kuandika maelezo ya ungamo( kutubu), alitishiwa iwapo atashindwa kusaini maelezo ya polisi, ataendelea kumteswa,” alidai wakili Nkwera.

Alidai mteja wake alimwambia alipoenda kwa mlinzi wa amani ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ukonga, alikuta maelezo ya onyo hayo na kulazimishwa kuyasiani.

Alidai, hata alivyokuwa Polisi, Kambi aliteswa na kulazimishwa kutoa maelezo, ambapo kwa upande wa washtakiwa waliosalia ambao hawakuwa na wakili wa kuwatetea,  kila mmoja alisimama na kutoa maelezo yake.

Mshtakiwa wa pili, Muharami maarufu kama Shilton, yeye alidai alipata kipigo na kudhalilishwa utu wake mbele ya wanawake akiwa uchi wa mnyama.

Bila kutaja sehemu anayodaiwa kufanyiwa uzalilishaji huo, Shilton alidai baada ya kukamatwa alilazimishwa kusaini maelezo ya onyo ambayo hakuyatoa.

“Nilipata kipigo na kudhalilishwa mbele ya wanawake nikiwa uchi wa mnyama,” alidai Muharami huku akiinama chini na kutikisa kichwa.

Muharami alidai alipopelekwa kwa mlinzi wa amani, aliandika maelezo na kumuonyesha makovu yake yaliyotokana na kipigo.

“Niliwauliza kama watanirudishwa tena pale pale mahabusu, wakasema ndio…nikasema wataniua,” alidai Muharami.

Mshtakiwa wa tatu, Maulid Mzungu, ambaye ni kaka mkubwa na  Muharami, alidai alipigwa kama walivyopigwa wenzake na kulazimishwa kusaini maelezo ya onyo ambayo hakuyatoa.

Mshtakiwa wa nne, Said Matwiko, yeye alidai akiwa kituo cha Polisi, bila kukutana jina, alisaini karatasi nyingi zisizokuwa na maandishi.

“Novemba 21, 2022 nilisaini pia karatasi nyingine nikiwa Mahakama ya Kisitu na kwamba makaratasi hayo nilisaini kwa lengo la kumwachia huru mke wangu, iwapo nitatekeleza hayo waliyokuwa wamenielekeza,” alidai Matwiko.

Kwa upande wa mshtakiwa wa tano, John Andrew maarufu Chipanda alidai alisanishwa kituo cha Polisi vitu ambavyo havifahamu.

“Mheshimiwa hakimu, nilivuliwa nguo na kufungwa bomba na kisha kuning’inizwa juu kichwa chini ili niseme ukweli,” alidai Andrew na kuongeza;

“Walisema hawana hasara ya kunipoteza kwa sababu taifa halitapata hasara yoyote.”

Kwa upande wa mshtakiwa wa sita ambaye ni mwanamke pekee kati kesi hiyo, Sara Joseph, yeye alidai kuwa walimchukua mume wake( Matwiko) nyumbani kwake na baadae maofisa wa DCEA walirudi na nyumbani kumchukua na yeye.

“Walivyokuja kunichunia mimi pale nyumbani, hawakunisainisha chochote na sijawahi kusaini kitu chochote hadi naletwa Mahakamani hapo,” alidai Sara.

Hata hivyo, washtakiwa hao walidaiwa kuwa watakuwa na mashahidi kila mmoja.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo ya mashahidi na vielelezo vya upande wa mashtaka pamoja na madai ya washtakiwa aliihamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Mkoa wa Dar es Salaam ( Kisutu) kwenda Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwa.

Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za Uhujumu Uchumi, isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP). Hivyo kesi za aina hivyo zinapokamilika hatua ya awali ya usikilizwaji wa maelezo ya mashahidi na vielelezo huamishiwa mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

Katika maelezo ya mashahidi, yaliyotolewa mahakamani hapo, uchunguzi wa Sayansi  Jinai uliofanywa na Jeshi la Polisi katika simu ya Kambi uliionyesha katika kitabu cha simu (Notebook) cha Kambi kilionyesha mawasiliano ya kupiga na kupigiwa kwa jina la Chipa( Chipanda), pia kulikuwa na sms za kutuma na kupokea.

Kwa upande wa simu ya Muharami, eneo la kitabu cha simu yake (Notebook) ilikuwa na maelekezo ya kugawana mzigo.

Related Posts