Walimu 12,000 kuajiriwa mwaka huu wa fedha

Dodoma. Wakati Tanzania ikiwa na upungufu wa walimu 271,025 kuanzia ngazi ya awali, msingi hadi sekondari kwa mujibu wa Tamisemi, Serikali imesema katika mwaka wa fedha 2023/24 itaajiri  walimu 12,000 ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu.

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 9, 2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Nora Mzeru.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itaajiri walimu wa kutosha kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, Serikali iliajiri walimu 29,879 wakiwemo walimu 16,598 wa shule za msingi na walimu 13,281 wa shule za sekondari.

Amesema mwaka 2023/24 Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu ili kukabiliana na hali hiyo.

Katika swali la nyongeza Nora amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira na kuwapa motisha walimu hasa wanaofanya kazi vijijini.

“Hili ni muhimu ili kuzuia walimu wengi wanaokimbilia mijini na kusababisha upungufu wa walimu vijijini,” amesema.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema hoja ya mbunge huyo ni muhimu na Serikali inatambua umuhimu wa motisha kwa walimu hasa  wanaofanya kazi vijijini ili wafanye kwa amani.

Amesema mkakati wa Serikali ni kujenga nyumba za kuishi ili kuboresha mazingira yao ya vijijini na kwamba katika mwaka 2022/23 wamejenga nyumba 253 ambazo zinabeba familia mbili kila moja.

“Serikali imeendelea kuhakikisha walimu wanalipwa malimbikizo  na stahiki zao kwa wakati na katika mwaka 2022/23, Serikali imelipa malimbikizo yasiyo ya mishahara ya Sh22.73 bilioni,” amesema.

Amesema hiyo ni mikakati inayofanywa, na Serikali inaendelea kufanya ili kuhakikisha kuwa watumishi wanaofanya kazi vijijini wanakuwa na  hamasa.

Related Posts