TANZANIA YAZINDUA MKAKATI MAALUM KUHAMASISHA MATUMIZI ENDELEVU YA NISHATI MBADALA

Na Seif Mangwangi,Arusha

SERIKALI ya Tanzania imezindua rasmi mkakati maalum wa matumizi sahihi na endelevu ya nishati mbadala ikiwa ni mwendelezo wa mkakati wa serikali wa kutokomeza matumizi ya kuni na mkaa ili kuokoa mazingira.

Uzinduzi huo ambao umeenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano wa kikanda wa matumizi sahihi ya nishati umefanyika leo jijini hapa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkakati huo Dkt Biteko amesema wadau mbalimbali wa Serikali na taasisi binafsi wanatakiwa kuungana kwa pamoja kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati sahihi ambayo gharama zake ni nafuu kulinganisha na nishati zingine.

Amesema Serikali ya Tanzania imeamua kuionyesha dunia kuwa inaunga mkono ajenda ya Dunia juu ya matumizi sahihi ya nishati na iko tayari kuungana na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kama ulivyokusudiwa.

Dkt Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapewa elimu kuhusiana na matumizi sahihi ya nishati ili kuhakikisha wanaepuka na gharama kubwa za nishati.

Amesema lengo la mkutano huo ambao umeandaliwa na Wizara ya Nishati kwa ushirikiano na Shirika la Kimataia la Maendeleo (UNDP), umoja wa Ulaya na ubalozi wa Ireland ni kujenga uelewa na kubailishana uzoefu katika masuala ya matumizi bora ya Nishati baina ya wadau kutoka ukanda wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
“Mkutano huu unafanyika ukiwa unatukumbusha kwamba suala la matumizi sahihi ya nishati sio suala la hiyari tena bali ni suala la lazima na linalohitajika kupewa kipaumbele na kuhakikisha nishati ya uhakika inapatikana, kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, na kukuza ukuaji endelevu wa uchumi,”amesema.

Kaimu Mwakilishi msaidizi Mkazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP, Amon Manyama amesema umoja wa Mataifa utaendelea kutoa msaaa wake kwa Serikali ya Tanzania na wadau wa maendeleo nchini kuhakikisha malengo ya matumizi ya nishati mbadala yanatekelezwa.
Amesema Serikali ya Tanzania ni mfano wa kuigwa dhidi ya Serikali zingine kuhusiana na namna ilivyopokea ajenda ya kimataifa ya kuhakikisha wananchi wake wanatumia nishati nafuu kupikia na kuwapunguzia gharama za maisha ikiwa ni pamoja na kuwajenga kiuchumi.


Related Posts