SERIKALI KUENDELEA KUJENGA UWEZO WA UFANYAJI WA TATHMINI ZA PROGRAMU NA MIRADI KWA WATAALAMU WA UFUATILIAJI NA TATHMINI NCHINI KWA VITENDO

Na Mwandishi wetu-Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini na Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Sakina Mwinyimkuu ameeleza kwamba Serikali imedhamiria kujenga uwezo wa kufanya Tathmini za Programu na Miradi kwa vitendo kwa kutumia Programu halisi zinazotekelezwa Nchini.

Mkurugenzi huyo alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku nne yanayofanyika katika Ukumbi wa Best Western Jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini kujifunza kwa vitendo namna ya kufanya Tathmini.

Alisema katika kutekeleza hilo, mafunzo maalum kwa wataalamu wa Ufuatiliaji na Tathmini yameanza kutolewa ambapo washiriki watapata fursa ya kujifunza namna ya kufanya Tathmini za Programu ambapo kwa kuanzia washiriki watatumia Programu ya Uendelezaji wa Kilimo nchini (ASDP II) nchini

“Programu hii inalenga kuboresha Sekta ya Kilimo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuboresha maisha ya mkulima wa Tanzania na kuwa na kilimo endelevu nchini,” Alisema Bi. Sakina.

Pia aliongeza kwamba Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo Awamu ya II ni programu ya kimkakati inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu nchini Tanzania.

“Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo ya Tathmini ya Ujerumani (DEval) na Kituo cha Kujifunza Tathmini na Matokeo cha Afrika ya Kusini ((CLEAR – AA) wameandaa warsha ya kujengea Taasisi za Umma katika kufanya Tathmini za Miradi na Programu mbalimbali,”Alisema Bi. Sakina.

Aidha Alieleza kuwa Utekelezaji wa programu hiyo unaonyesha juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuongeza kipato cha mkulima mmoja mmoja na kuwezesha ukuaji wa Uchumi wa Taifa kwa ujumla.

“Mafunzo haya ni mwanzo wa Mafunzo ya vitendo yatakayoendelea kutolewa kwa watumishi wa Umma na kujifunza namna ya kufanya Tathmini za Miradi na programu kwa vitendo,” Alibainisha.

Related Posts