Kagoma avunja ukimya ishu na Simba

WAKATI taharuki ikiendelea kutanda juu ya kiungo wa Simba, Yusuph Kagoma kufuta picha na utambulisho wa kuwa ni mchezaji wa timu hiyo katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Instagram,  mwenyewe amevunja ukimya na kuanika sababu ya kufanya hivyo.

Kagoma, ni kati ya wachezaji wa Simba waliobaki nchini wakati timu hiyo ikiwa Algeria kucheza mchezo wa pili wa Kundi A ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Costantine itakayopigwa Jumapili na akizungumza na Mwanapoti mapema leo amesema ameamua kujiondoa kwa muda katika mitandao ya kijamii.

“Hakuna ishu yoyote kubwa, nimeamua kuacha kutumia Instagram kwa muda, ila mimi bado ni mchezaji halali wa Simba kwa mujibu wa mkataba niliosaini mwanzoni mwa msimu huu,” amesema Kagoma na kuongeza;

“Kuhusiana na suala la kubaki Tanzania wakati timu ipo Algeria, mimi nilikuwa naumwa nimerudi kuanza mazoezi siku nne kabla ya timu kusafiri hivyo bado sipo fiti.”

Kagoma amesema wakati timu inaondoka, ameachiwa programu maalumu na benchi la ufundi ili kujiweka fiti na anaweza akawa sehemu ya mchezo unaofuata wa michuano hiyo dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia mchezo utakaopigwa Desemba 15 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Kiungo huyo wa zamani wa Geita Gold na Singida Fountain Gate, amesema anaitakiwa kila la kheri chama lake la Simba kwa mchezo huo wa Jumapili, huku akiweka wazi, anaamini kikosi kilichosafiri kwenda Algeria kinaweza kufanya vizuri na kuipa timu hiyo matokeo mazuri kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Simba iliishinda Bravos do Maquis ya Angola kwa bao 1-0. Bao lililofungwa kwa penalti na Jean Charles Ahoua.

Kagoma hajaonekana uwanjani tangu Oktoba 19 wakati pambano la Dabi ya Kariakoo, baada ya kuumia na kutolewa wakati Simba ikilala bao 1-0 Kwa Mkapa kwa bao la kujifunga la beki wa kulia wa timu hiyo, Kelvin Kijiri dakika za lala salama.

Related Posts