17 Coastal wasikilizia pingamizi la uchaguzi

SIKU chache baada ya Kamati ya Uchaguzi ya klabu ya Coastal Union kutangaza majina 17 ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, kwa sasa wanasikilizi siku mbili kuwekewa pingamizi kabla ya kuanza kampeni na kusubiri maamuzi ya sanduku la kura siku ya Desemba 21.

Muda wa pingamizi kwa wagombea hao waliopenya kutokana na kukidhi sifa na vigezo vya kushiriki uchaguzi huo, huku wenzao waliojitokeza awali kutemwa umeanza leo Ijumaa na utafikia tamati keshokutwa Jumapili.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa sasa wa klabu hiyo kupitia Idara ya Habari, inaeleza Desemba 8-12 itakuwa ni siku za rufaa kwa wagombea watakaokuwa wamewekewa pingamizi ambapo rufaa hizo zitasikilizwa na Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Siku ya Desemba 14 wagombea na Kamati ya Uchaguzi watajulishwa uamuzi wa Kamati ya Rufaa na uchaguzi kabla ya Desemba 16 kupitisha orodha ya mwisho ya wagombea na kubandika katika ubao wa matangazo kisha Desemba 17-20 itakuwa ni siku za kampeni na Uchaguzi Mkuu utafanyika Desemba 21.

Awali wagombea 25 walijitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uchaguzi huo kisha wanane kuchujwa kwa kukosa vigezo na sifa kupitia kwenye usaili na kubakiza hao 17.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Coastal, Wakili Emmanuel Kiariro alisema nafasi ya Mwenyekiti iliyokuwa inawaniwa na wajumbe wawili, lakini kwa sasa amebaki mmoja baada ya Abdurahman Fumbwe kuenguliwa kwa kigezo cha kutokukidhi kanuni  ya 9 (6) ya kanuni za uchaguzi  za wanachama.

Wakili Kiariro alisema katika nafasi ya Ujumbe Kamati ya Utendaji wameenguliwa wagombea saba kutokana na kushindwa kukidhi kanuni mbalimbali za uchaguzi.

Aliwataja walioenguliwa ni; Khamis Karim Khamis, Thabit Mwinyi Abuu, Ahmed Awadh Ahmed, hajakidhi kanuni ya 9 (6) ya kanuni za uchaguzi za wanachama toleo la 2021, Ally Hussein Kingazi, Abdullah Mbaruk Andullah,Salum Juma Mwawado, Omar Mtunguja Kombo hajakidhi kanuni ya 9 (7) ya kanuni za uchaguzi za wanachama toleo la 2021.

Wakati huo huo Kiariro amewataja wagombea wa nafasi mbalimbali waliopitishwa hukub nafasi ya mwenyekiti akibaki mmoja ambaye ni Hassan Ramadhan Muhsin, nafasi ya makamu mwenyekiti inagombewa na Dk. Fungo Ali Fungo na Mohammed Kiruasha Mohammed.

Nafasi ya wajumbe waliobaki ni Hussein Abdallah Moor, Khamis Seleh Khamis, Emmanuel Abdallah Mchechu, , Saida Said Bawazir, Nassor Mohammed Nassor, Hafidh Nassor Suleiman,  Abdallah Zubeir Unenge, Mohammed Maulid Rajab, Baraka Mohammed Baraka, Injinia Baraka Fumbwe, Ally Saleh Sechonge,Hussein Ally Mwinyihamis, Sudi Said Hilal na Wazir Mohammed Wazir.

Related Posts