Yanga ilivyowapiga bao Waarabu | Mwanaspoti

Yanga itacheza mchezo wa pili wa makundi ya Klabu Bingwa Afrika kesho Desemba 7, 2024 dhidi ya MC Alger kwenye uwanja wa Julai5, 1962 huku ikipewa nafasi kubwa ya kupata matokeo kutokana na takwimu mbaya za wapinzani wao wakiwa katika uwanja wa nyumbani.

MC Alger imecheza michezo 10 ya Ligi ikiwa imeshinda mechi nne, imetoa sare tano, huku ikifungwa mechi moja ambapo imecheza mechi tano kwenye uwanja wa nyumbani ikiwa imeshinda mechi moja, imetoa sare mechi tatu na kupoteza mchezo mmoja ikivuna pointi sita kati ya 15 ilizotakiwa kupata kwenye mechi tano za nyumbani.

Kwenye michezo mitano iliyocheza ikiwa ugenini MC Alger imeshinda mechi tatu, imepata sare mechi mbili ambapo imevuna pointi 11 kati ya 15 ikiwa imekusanya pointi nyingi tofauti na michezo iliyocheza ikiwa nyumbani.

Mchezo mmoja ambao MC Alger ilishinda ikiwa nyumbani iliifunga El Bayadh bao 1-0 ambayo inabuluza mkia nafasi ya 16 ikiwa na pointi nane ambapo mechi nyingine ilifungwa na CR Belouzidad mabao 3-1.

Upande wa ufungaji mabao MC Alger imefunga mabao matatu ikiwa nyumbani huku ikiruhusu kufungwa mabao manne wakati ikiwa ugenini imefungwa mabao mawili huku yenyewe ikifunga mabao matano ambapo jumla inakuwa imefunga mabao nane huku ikiruhusu mabao sita.

Mabingwa hawa watetezi wa Algeria msimu uliopita walimaliza michezo ya Ligi kuu ambapo walikusanya pointi 65 katika michezo 30 huku wakipachika mabao 55 wakiruhusu mabao 20.

Youcef Belaïli ambaye alikuwa mfungaji bora wa Algeria akifunga mabao 14 aliisaidia MC Alger kubeba Ubingwa wa Ligi ambapo msimu huu anakosekana baada ya kutimkia kwa vigogo wa Tunisia Esperance de Tunis, hii inakuwa faida kwa Yanga ambayo imefanikiwa kubakiza nyota wake muhimu kikosini waliyofanya vizuri msimu ukiopita.

Uwepo wa Stephan Azizi Ki, Pacome Zouzoua, Max Nzegeli, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Djigui Diarra, Kouassi Yao pamoja na Clement Mzize ambao waliitajika na vilabu vikubwa hapa Afrika pengine inaweza kuwapa faida kwa Yanga kuwa na wachezaji wenye uzoefu kwenye mashindano na wanaojuana wakiwa uwanjani.

MC Alger ambayo imewauza baadhi ya nyota wake kwenye vilabu vingine ikiwa imeleta wachezaji wengine ambao wanaitaji muda kuzoeana ambapo imeonekana wazi kabisa wakipitia nyakati ngumu kupata matokeo ata wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Hivyo ni fursa kwa Yanga kucheza kimkakati ili kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu ugenini wakiwa walishafanya hivyo dhidi ya timu za Waarabu kama USM Alger na Club Afrcain.

MC Alger inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 17 kwenye msimamo wa Ligi kuu Algeria ambapo nafasi ya tatu inashikwa na USM Alger ikiwa na pointi 16 sawa na USM Khenchela yenye pointi 16 ikiwa nafasi ya nne huku nafasi ya kwanza inashikwa na wapinzani wa Simba, SC Constantine yenye pointi 19.

Related Posts