Na Mwandishi wetu, Mpapura
Afisa Tarafa Mpapura Emmanuel Shilatu amewapongeza Walimu, Wanafunzi na Wazazi kwa jitihada kubwa wanazoweka zinazopelekea kupata mafanikio makubwa ya ufaulu.
Pongezi hizo Shilatu ambaye alikuwa Mgeni rasmi amezitoa wakati akizungumza kwenye Mahafali 16 ya kidato Cha nne Shule ya Sekondari ya Libobe iliyopo Kata ya Libobe, Tarafa ya Mpapura mkoani Mtwara ambapo jumla ya Wanafunzi 60 wamehitimu kati yao Wavulana ni 20 na Wasichana ni 40.
“Kipindi cha nyuma Shule za Kata zilikuwa zinaonekana hazina maana ila hali ya sasa ni tofauti kwani Shule zenye ufaulu mkubwa ni za Kata. Niwapongeze Shule ya Sekondari ya Libobe kwa namna mlivyoweza kuongeza ufaulu kwa haraka sana ndani ya muda mfupi hadi kuweza kushika nafasi ya 3 kwa ngazi ya Halmashauri na kwa mara ya kwa imepatikana Division I ya 13 kwa Mwanafunzi wa kike kwa matokeo ya kidato cha Nne mwaka Jana (2023). Hongereni sana uongozi wa Shule kwa mikakati, hongereni sana Wazazi kwa ushirikiano mnaoutoa, hongereni sana Wanafunzi kwa bidii zenu” alisema Gavana Shilatu.
“Pongezi na shukrani za kipekee zimwende Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotoa kipaumbele Sekta ya Elimu kwa kutoa fedha za uendeshaji na uboreshaji wa miundombinu na matokeo ni ubora wa Elimu na ufaulu kuongezeka kwa Shule za Serikali, tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais Samia.” Alimalizia Shilatu.
Nae Mkuu wa Shule Sekondari Libobe Mwalimu Urban Makota aliipongeza Serikali kwa usimamizi na Wazazi kwa ushirikiano unaopelekea ufaulu kuongezeka.
“Mwaka Jana Mwanzoni ukiwa bado mgeni ulikuja shuleni ukatusema sana juu ya matokeo mabaya tuliyoyapata, ulitufuatilia sana sisi ambao hatukuwa na ufaulu mzuri, Leo hii tunaona matunda yake. Tunawashukuru pia Wazazi kwa namna walivyo tuunga mkono tulipokuja na mikakati ya kuboresha Elimu, Leo hii wanafurahia kuona Watoto wao wanafanya vizuri kitaaluma. Tuendelee kushirikiana ili tuendelee kufaulu zaidi na zaidi.” Alisema Mwl Makota.
Nao Wazazi wa Wanafunzi wameishukuru Shule ya Sekondari Libobe kwa kuwalea na kuwasomesha Watoto wao kwa ubora. Pia wamemshukuru Rais Samia kwa namna anavyoboresha Elimu kwani amekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya Watoto wao.