Dar es Salaam. Watu sita Wakazi wa jijini hapa wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni iliyopo Kinondoni, wakikabiliwa na shtaka la kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo.
Washtakiwa hao waliopandishwa kizimbani ni pamoja na Fredrick Juma Said mjasiriamali, Isack Mwaifani, Benki Mwakalebela, Mkazi wa Mbezi Makabe na wakala stendi ya Magufuli; Bato Bahati Tweze (32) mkazi wa Kimara; Nelson Elimusa, dereva teksi na Anita Temba, mkazi wa Mbezi Mwisho.
Washtakiwa hao wamesomewa shtaka moja leo Ijumaa Desemba 6, 2024, la kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo kwa nia ya kumweka kizuizini isivyo halali, kinyume na vifungu vya 380 (1) na 381 (1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali John Mwakifuna ameieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 11, 2024, eneo la Kiluvya Madukani Lingwenye jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa wote wamekana shtaka hilo na Wakili Mwakifuna ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na akaomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya usikilizwaji awa awali.
Washtakiwa wote wameomba dhamana na Wakili Mwakifuna akasema kwa hana pingamizi kwa kuwa shtaka lao linadhaminika.
Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira amewaeleza washtakiwa kuwa dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kusaini bondi ya dhamana ya Sh20 milioni kila mmoja.
Masharti mengine ya dhamana ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka kwa waajiri wao, kama ni waajiriwa, au kutoka Mtendaji wa Kata.
Pia hawatakiwi kutoka nje ya Mkoa bila ruhusa ya Mahakama.
Hakimu Rugemalira ameahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 19, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali na usikilizwaji kamili.
Washtakiwa hawakutimiza masharti ya dhamana na wamepelekwa mahabusu.