MSHAMBULIAJI wa KMC, Daruweshi Saliboko amesema Ligi Kuu Bara imechangamka hasa eneo la ufungaji mabao, jambo linalompa nguvu kuona nafasi ya kuwania kiatu cha ufungaji bora ipo wazi msimu huu.
Saliboko aliyemaliza na mabao manne na asisti tatu msimu uliopita, alisema akimtazama kinara wa mabao sita ambaye ni Selemani Mwalimu wa Fountain Gate anaamini hawajapishana sana na wale waliopo chini yake.
“Tofauti na msimu uliopita ilikuwa ni Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salim ‘Fei Toto’ kwenye ushindani wa kufunga mabao, ingawa walikuwepo wengine ambao walikuwa wanafunga, lakini awamu hii mambo ni tofauti kabisa,” alisema.
“Hatujazidiana idadi kubwa ya mabao aliyeko chini anaweza akapanda juu, kikubwa ni kuendelea na mapambano kila kitu kinawezekana.”
Mara ya mwisho Saliboko kufunga mabao mengi (12) ilikuwa msimu wa 2019/20 akiwa Lipuli ya Iringa, lakini hajaifikia hadi sasa na akizungumzia hilo alisema ni kutokana na kubadilishiwa majukumu na kocha Malale Hamsini alipokuwa Polisi Tanzania.
“Wakati najiunga Polisi 2020/22 kuna mshambuliaji alikuwa anacheza namba tisa na alikuwa anafanya vizuri, hivyo akasema nicheze winga kuisaidia timu. Msimu huo nilimaliza na mabao saba, uliofuata nikamaliza na matatu,” alisema.
“Kisha nikajiunga na KMC 2022/23 nikamaliza na mabao sita na uliopita nilimaliza na mabao manne na asisti tatu,ukicheza namba tisa ni rahisi sana kufunga kwani unakuwa unakaa karibu na goli.”
Mbali na kuota tuzo ya ufungaji bora, Saliboko pia alimtaja kiungo mshambuliaji wa Yanga, Clatous Chama namna anavyocheza kwa utulivu wakati wa kutoa pasi hadi anapofika golini, anakuwa hana papara ya kufunga.
“Ukiachana na Chama napenda aina ya uchezaji wa Fei Toto pia ni mtulivu ana uwezo wa kufunga mabao ya mbali, katunza kiwango chake ndio maana muda wote anaocheza Ligi Kuu ni msaada kwa timu anazokuwepo.”