Dar es Salaam. Kwa takribani miaka tisa wanawake zaidi ya 300 waliopata changamoto ya kukakamaa sehemu mbalimbali za mwili au kupata majeraha makubwa yaliyosababishwa na vitendo vya ukatili, ajali au maradhi mbalimbali wamerejeshewa tabasamu baada ya kufanyiwa bure upasuaji rekebishi katika hospitali ya Aga Khan.
Kwa mwaka 2024 pekee wanawake 27 wamefanikiwa kupata huduma hiyo ya upasuaji iliyoanza kutolewa kuanzia Novemba 29 hadi Disemba 6.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Disemba 6, 2024 jijini Dar es Salaam, Dk Athar Ali, daktari bingwa wa upasuaji na mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, amesema kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ajali na maradhi mbalimbali ikiwemo saratan, wanawake wanaweza kupata majeraha yanayosababisha uharibifu wa viungo au ulemavu.
Dk Ali amesema kutokana na majeraha hayo, wanawake walioathiriwa wanaweza kushindwa kuteketeleza kikamilifu majukumu yao ya kila siku kwa upande wa familia na shughuli za kiuchumi.
βUpasuaji huo unalenga kurejesha uwezo wa kutembea na kukunjua viungo vilivyokakamaa kwa wanawake na wasichana kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, ambao wamepata ulemavu wa kutembea kutokana na majeraha ya moto, ukatili wa kijinsia, ajali na kukosa uwezo wa kumudu gharama hizo za upasuaji rekebishi,β amesema.
Anaeleza kuwa upasuaji huo umefanywa na Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa kushirikiana na Reconstructing Women International (RWI) na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
βKatika awamu tisa zilizopita tangu tulipoanza programu hii mwaka 2016 zaidi ya wagonjwa 300 wamenufaika na upasuaji huu wa bure. Pia madaktari 16 wa upasuaji wa kurekebisha, upasuaji wa jumla na wanafunzi wa tiba kutoka hospitali mbalimbali za umma na binafsi wamepata mafunzo kupitia mpango huu.”
Amesema kutokana na kuwepo idadi kubwa ya watu wanaohitaji kupatiwa huduma hiyo, wanatarajia kuanza kuitoa mara mbili kwa mwaka baada ya mara moja kama ilivyokuwa awali.
Dk Edwin Mrema, daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha mwili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema kadri idadi ya watu nchini Tanzania inavyoongezeka, mahitaji ya huduma maalumu za afya, ikiwa ni pamoja na upasuaji huo, yanazidi kuongezeka.
Ili kukabiliana na hili, Serikali inashirikiana na watoa huduma binafsi kama Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam na mashirika ya kimataifa kama Reconstructive Women International (RWI).
βUshirikiano huu unalenga kujenga uwezo wa madaktari wa ndani, kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kisasa na kuleta madaktari wataalamu kutoka nje ya nchi,” amesema.
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha mwili na kiongozi wa timu ya RWI, Dk Andrea Pusic, amesema ushirikiano kati yao umewezesha kutoa huduma kwa wanawake na wasichana wengi wenye shida hiyo.
Daktari bingwa wa upasuaji na upasuaji kwa matundu madogo katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Aidan Njau amehimiza wananchi kutumia vyema fursa hizo za matibabu bure zinapojitokeza, kwani kwa kawaida huwa na gharama kubwa.