Waasi wa Syria waendelea kusonga mbele – DW – 06.12.2024

Muungano wa waasi hao unaoongozwa na kundi lenye itikadi kali la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) wameendelea kupambana na vikosi vya serikali upande wa kusini baada ya kuchukua udhibiti wa mji wa kaskazini wa Aleppo na ule wa Hama uliopo katikati mwa nchi hiyo. Hali ambayo ilikuwa haijashuhudiwa tangu mwaka 2011 vilipomalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kufikia leo asubuhi, waasi hao walikuwa kilomita tano tu karibu na mji mwingine muhimu wa Homs  baada ya kuiteka miji miwili midogo ya Rastan na Talbiseh. Hii ikiwa ni kulingana na Shirika la Kufuatilia vitendo vya Haki za Binadamu nchini Syria ambalo lilisema kuwa jeshi la taifa lilijiondoa kwenye mji huo, taarifa iliyokanushwa na wizara ya Ulinzi ya Syria.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: ANKA

Iwapo waasi watauteka mji huo wa Homs, itamaanisha kuwa Assad hatokuwa tena na udhibiti katika eneo la pwani ya bahari ya Mediterania, ambalo ni ngome muhimu ya ukoo wake ulioitawala Syria kwa miongo mitano iliyopita. Mkuu wa kundi hilo la waasi amesema wanalenga kusonga mbele hadi mji mkuu Damascus na kuuangusha utawala wa Assad.

Kauli za mataifa ya kigeni yanayohusika kwenye  mzozo huo wa Syria  zimetolewa. Baada ya sala ya Ijumaa, rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema anatumai kuwa waasi hao wataendelea vyema na harakati zao dhidi ya vikosi vya Rais Bashar al-Assad lakini akadhihirisha wasiwasi wake kuhusu uwepo wa magaidi miongoni mwa waasi hao.

” Kwa sasa, wanailenga Idlib, Hama na Homs. Lakini lengo kuu ni Damascus. Harakati hizi za upinzani zinaendelea hivi sasa, na tunazifuatilia kupitia taarifa za kijasusi na vyombo vyote vya habari. Bila shaka, nia yetu ni kuona harakati hizi huko nchini Syria zinaendelea bila tatizo lolote, ” alisema Erdogan.

Iran, Urusi zaendelea kuinga mkono serikali ya Assad

Rais wa Urusi Vladimir Putin akisalimiana na mwenzake wa Iran Masoud Pezeshkian
Rais wa Urusi Vladimir Putin akisalimiana na mwenzake wa Iran Masoud PezeshkianPicha: Alexander Shcherbak/SNA/IMAGO

Rais Bashar Al-Assad anawategemea washirika wake wakuu ambao ni Urusi na Iran. Serikali mjini Tehran imesema hivi leo kuwa itatuma nchini Syria makombora, droni na wataalam wa kijeshi ili kuendelea kumsaidia rais huyo wa Syria kupambana na waasi hao.

Shirika la habari la serikali ya Urusi TASS limeripoti kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi, Uturuki na Iran wanatarajiwa kukutana kwa mazungumzo hapo kesho mjini Doha nchini Qatar na kuijadili hali inayoendelea huko Syria.

Soma pia: Umoja wa Mataifa watoa wito wa kupunguza uhasama Syria

Israel kwa upande wake imeimarisha usalama katika eneo la milima ya Golan inayopakana na Syria na kusema haitoruhusu wala kuvumilia vitendo vyovyote vitakavyoweza kuyumbisha usalama wa taifa lake. Jordan imetangaza kuufunga mpaka wake na Syria huku Urusi ikiwataka raia wake kuondoka nchini humo.

Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani amefanya mazungumzo na wanadiplomasia wa Syria na Iran huku akitoa wito kwamba nchi yake inasisitiza juu ya umuhimu wa kuendeleza juhudi za kidiplomasia zinazolenga kuudhibiti mgogoro wa Syria kutokana na athari zake za wazi kwa usalama wa eneo hilo la Mashariki ya Kati.

(Vyanzo: AP, Reuters, DPAE, AFP)

 

Related Posts