Rais kutwaa ardhi Dar es Salaam

Dodoma. Serikali imetangaza kusudio la kutwaa eneo la mita za mraba 233,000 katika Manispaa za Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam.

Eneo hilo imeelezwa litatumika kwa ajili ya hifadhi  ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart).

Tangazo la kusudio la kutwaliwa eneo hilo limetolewa Novemba 6, 2024 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali la Novemba 29, 2024.

“Tangazo linatolewa kwamba Rais anakusudia kutwaa kwa manufaa ya umma ardhi ya ukubwa wa mita za mraba 233,000 zilizopo katika Manispaa ya Kinondoni na Ubungo Mkoa wa Dar es Salaam na linahusisha makazi ya watu katika makutano ya barabara ya Bagamoyo na Kunduchi (Mbuyuni),” imeelezwa katika tangazo hilo.

Maeneo mengine yanayohusishwa katika tangazo hilo ni Sam Nujoma na Chuo Kikuu cha Ardhi mkabala na Mlimani City na eneo linalomilikiwa na Manispaa ya Ubungo lililopo Simu2000 na Boko Basihaya.

Tangazo hilo limesema mtu yeyote anayedai kuwa na haki yoyote katika ardhi hiyo anatakiwa kutoa maelezo ya uthibitisho wa haki hiyo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndani ya majuma sita kutoka tarehe ya tangazo hilo kutolewa katika gazeti la Serikali.

“Inatangazwa pia kwamba kama Rais hakuagiza vinginevyo kuhusu siku ya kuingia katika ardhi hiyo, ananuia kuingia katika ardhi hiyo yatakapoisha majuma sita tangu tarehe ya kutolewa kwa tangazo hilo katika gazeti la Serikali,” imeelezwa.

Imeelezwa mtu yeyote ambaye kwa hila au kwa makusudi atamzuia mtu yeyote ambaye amepewa madaraka ipasavyo kisheria iliyotajwa hapo juu, atalazimika kulipa faini isiyozidi Sh5,000 au kufungwa kwa muda usiozidi miaka miwili au vyote faini na kifungo.

Taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinasema maeneo hayo yatatumiwa kwa ajili ya miundombinu ya Dart.

Maeneo yanayotwaliwa yamegawanywa katika makundi matatu ambayo Simu 2000 zinatwaliwa mita za mraba 35,000 kwa ajili ya ujenzi wa karakana, Sam Nujoma na Chuo Kikuu cha Ardhi mkabala na Mlimani City (24,000) ambalo kitajengwa kituo cha maegesho ya mabasi.

Mita za mraba 156,000 katika makutano ya barabara ya Bagamoyo na Kunduchi Mbuyuni kutajengwa karakana kuu.

Alipotafutwa Mkurugenzi Mkuu wa Dart, Athuman Kihamia amesema maeneo hayo yatatumika kama eneo la kuhifadhia.

Kuhusu fidia kwa wamiliki wa maeneo yanayotwaliwa, Kihamia amesema kwa sasa hawawezi kutaja watu watakaopata fidia kwa sababu ni mtu mmoja.

“Wanaofanya tathimini ni Mthamini Mkuu wa Serikali akishirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na sisi tutafanya malipo baada ya kukamilika kwa tathmini,” amesema.

Related Posts