Dk Biteko akemea migogoro ndani ya vyama vya wafanyabiashara

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amevitaka vyama vya kisekta ikiwemo Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kuepuka migogoro ya ndani ili vyama vyao viwe na tija.

Badala yake amevitaka vyama hivyo kukumbushana umuhimu wa kulipa kodi ili kuchagiza maendeleo ya nchi.

Biteko ametoa kauli hiyo leo katika kongamano la majadiliano ya biashara kati ya Serikali na sekta binafsi, ambayo yameunganishwa na mkutano wa 49 wa TCCIA.

Mkutano huo umekutanisha wadau wa sekta binafsi na umma pamoja na wanachama wa TCCIA kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara, ukilenga kujadili maendeleo ya kilimo, viwanda na biashara nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Dk Biteko amewataka watu walio ndani ya vyama hivyo, kuepuka migogoro na kupendana huku akisema wakati mwingine badala ya kujibu shida za wanachama wake, vyama hivyo hugeuka kuwa vya harakati.

“Na chama kikiwa cha harakati anayepata heshima ni kiongozi wa chama, akisimama kwenye TV atatajwa yeye na si chama chenu,” amesema Dk Biteko.

Alitumia nafasi hiyo kuvitaka vyama hivyo kusimamia umoja na kupendana.

“Wakati mwingine rais wenu anaweza kuwa na makwazo lakini ni vyema kutambua kuwa huyo ni binadamu aliyezaliwa na mwanamke, mwenye matatizo mengi anayoyajua na asiyoyajua,” amesema Biteko na kuongeza:

“Sasa katika hali kama hii ni vyema mumfanye awe rais bora kwa manufaa ya chama chenu, akitokea mtu miongoni mwenu ambaye hakubaliani na yeye akaenda kuzungumza mambo yenu nje ya mfumo wa vikao, nia yake si njema ni kuua hicho chama.”

Amesema ikiwa mtu ambaye anasababisha mfarakano akija kupata nafasi ya kuwa rais wa chemba, siku moja ataharibu kwa sababu dhambi aliyoipandikiza haitamuacha na gharama hiyo italipwa na chama, si yeye.

Dk Biteko alitumia nafasi hiyo kuitaka TCCIA kutumia mkutano huo kukumbushana kuwa wao wako kwa ajili ya kufanya bishara na Serikali ipo kwa ajili ya kuwasaidia.

Mbali na hilo aliwataka kuwa mstari wa mbele katika kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili waweze kuchangamkia fursa za kuzalisha bidhaa za ndani ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani, kikanda na kimataifa.

 “Pia niwakumbushe, akija mwekezaji wa nje asichukuliwe kama adui, bali mshindani ambaye atatusaidia kushindana kimataifa,” amesema Dk Biteko.

Amewataka kufanya biashara kwa ushindani kwani Serikali inawategemea wananchi wake kwa ajili ya kuleta maendeleo ya nchi.

Alitumia nafasi hiyo kuitaka TCCIA kuwa mawakala wa kutoa elimu ya mlipakodi kwa Watanzania huku akieleza kuwa ni raha kumlaumu mkusanya kodi lakini gharama yake ni kubwa ikiwemo kulalamikia huduma ambazo hazipatikani.

“Ninyi ni jeshi kubwa lililosambaa nchi nzima ambapo pamoja na kufanya biashara, mnatoa ajira kwa watu wengi na kazi ya serikali ni kuhakikisha mazingira ya wafanyabiashara yanakuwa mazuri,” amesema Dk Biteko.

Suala la migogoro lililozungumziwa na Naibu waziri mkuu liliwahi kutokea ndani ya TCCIA kiasi cha kufanya viongozi wake wa ngazi ya Taifa kutolewa na kuteuliwa viongozi wengine waliokaimu nafasi hizo hadi pale ulipofanyika uchaguzi kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

Uamuzi huo ulifanyika Mei 5, 2023 katika kikao cha Halmashauri Kuu taifa, na Mkutano Mkuu uliofanyika Morogoro huku sababu ikitajwa kuwa ni kuwapo kwa migogoro ndani ya chemba hiyo kwa miaka miwili, hali ambayo ilileta athari za kiutendaji.

Kuondolewa kwa viongozi hao kulitajwa kulinda masilahi ya chemba kuliko masilahi ya mtu mmoja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Oscar Kissanga amesema taasisi hiyo inalenga kuunganisha wadau wa biashara na kukuza sekta ya biashara na kilimo nchini.

“Katika kipindi cha miaka 36 TCCIA imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha ushindani na kuvutia wadau wa ndani na nje ya nchi,” amesema Kissanga.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Trademark Afrika, Elibariki Shammy amesema taasisi yake inalenga kuisaidia Watanzania na Afrika kwa ujumla ili iweze kufanya biashara na dunia.

Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Vicent Minja amesema tangu kuanzishwa kwake,  TCCIA haijawahi kuanzisha migomo kwa sababu kunapokuwa na changamoto imekuwa ikitafuta wahusika ili iweze kutatuliwa.

“Kwa sasa chama chetu kinafanya kazi katika mikoa 26 nchini na tumekuwa na mabaraza mbalimbali ya biashara ambayo pia yanahusika katika kutatua changamoto mbalimbali za wafanyabiashara,” amesema.

Related Posts