SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUTOA BILIONI 8 ,KUJENGA SHOPPING MALL KIBAHA MJINI

 

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, ameishukuru Serikali kwa kuipatia Halmashauri ya Kibaha Mji kiasi cha sh. bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kisasa la maduka makubwa (shopping mall), ambalo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi Disemba 7 mwaka huu.

Akizungumza wakati wa kikao cha ushauri cha Wilaya ya Kibaha, Nickson alisema kuwa mradi huo ni chachu ya maendeleo na hatua muhimu katika kuboresha sura ya mji huo.

“Jengo hili la maduka makubwa litatoa fursa kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa zao na kuchochea ukuaji wa kiuchumi.

” Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizi, ambazo zitazalisha ajira na fursa nyingi za kuwawezesha wananchi kiuchumi,” alisema Nickson.

Aidha, aliishauri Halmashauri ya Kibaha Mji kuridhia maombi ya Chuo cha Biashara (CBE) kufungua tawi mjini humo, akibainisha kuwa uwepo wa chuo hicho utachangia kuvutia uwekezaji wa vyuo vingine na kuinua maendeleo ya mji wa Kibaha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema jengo hilo litazinduliwa rasmi Disemba 7 mwaka huu, ambapo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon.

“Tayari jengo limekamilika na biashara zimeanza, Vyumba 64 vimeshapangishwa, lakini mahitaji ni makubwa na vyumba vilivyopo havitoshi.

Bidhaa zinazouzwa ni za kisasa na bei ni nafuu,” Tunawahimiza wananchi kujitokeza na kutuunga mkono,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Aidha, alisisitiza kuwa amepokea ushauri uliotolewa kwenye kikao hicho na ameahidi kuufanyia kazi.

Katibu wa Bakwata Kibaha, Ismail Danda, aliipongeza halmashauri kwa kurahisisha utoaji wa leseni za biashara, huku akihimiza zoezi hilo liwe endelevu ili kukuza sekta ya biashara wilayani humo.

Hamis Kazi ya Mungu pia alisifu hatua za maendeleo, hususan ujenzi na uzinduzi wa maduka hayo, na ametoa wito wa kushirikiana na vyama vingine vya siasa katika masuala ya maendeleo.

Mradi wa jengo hilo la maduka uligharimu shilingi bilioni 8, ambazo zilitengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019. Ujenzi huo ulitekelezwa na Mkandarasi Elerai Construction Co. Ltd na kusimamiwa na M/S Luptan Consult pamoja na Mhandisi Consultancy Ltd.

Related Posts