Dar es Salaam. Ukiukaji wa utaratibu wa ukamataji unaofanywa na vyombo vya dola, umezua hofu miongoni mwa wananchi, ambao wanauhusisha na matukio ya utekaji.
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka matukio ya watu kukamatwa yakihusishwa na utekaji, huku mengine yakihusisha watendaji wa vyombo hivyo.
Tukio la hivi karibuni ni la dereva ambaye kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi aliyepiga kelele, akidai anatekwa kwenye tukio lililosababisha wananchi kuwajeruhi watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Tukio hilo lilitokana na maofisa hao kulizuia gari alilokuwa anaendesha kwa ajili ya ukaguzi wa magari yaliyoingia nchini bila kulipiwa kodi.”
Kwa mujibu wa TRA, gari hilo aina ya BMW x6 lenye namba T239 DHZ lilibainika kutokuwa ndani ya mfumo wa TRA na watumishi hao walipojaribu kulizuia, kuliibuka mzozo hadi dereva akapiga kelele kuomba msaada, akidai anatekwa.
Kukamatwa kwa dereva huyo kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alipoulizwa na Mwananchi, leo Ijumaa, Desemba 6, 2024.
Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu utaratibu uliotumika kumkamata dereva huyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo amejibu kwa njia ya maandishi:
“Watumishi wa mamlaka hawakuwa kwenye ukamataji, bali walitaka kulikagua gari lile baada ya kubaini namba zake hazikuwa halali.
“Hiyo T 229 DHZ ni namba ya Nissan Civilian Bus siyo BMW na (dereva) hakukamatwa, bali alisimamishwa kwa ajili ya ukaguzi na baada ya kugundulika kosa lake hatua zaidi zingefuata, ikiwepo kuwashirikisha polisi kwa sababu namba bandia na mambo mengine ikiwemo gari kutumika kwenye uhalifu au ukwepaji wa kodi.”
Kayombo amesema watumishi waliojeruhiwa walikuwa maofisa wa forodha, waliotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Utawala wa Forodha wa Afrika Mashariki kuanzia kifungu 149 hadi 153.
Amesema maofisa hao wanapotekeleza majukumu yao hawahitaji kibali chochote cha mahakama.
Awali, taarifa ya TRA ilisema watumishi hao walijeruhiwa Desemba 5, 2024 wakiwa kwenye doria ya kudhibiti, ukamataji wa magendo na magari yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria.
Watumishi hao walilizuia gari hilo kwa mbele kwa gari aina ya Toyota Land Cruiser, huku wakimsihi dereva kuongozana nao, lakini alikataa akisema TRA hawafanyi kazi usiku, kwa mujibu wa mashuhuda.
Mashuhuda hao wamesema watumishi hao waliwapigia simu polisi kuomba msaada na wakati majibizano yakiendelea, dereva huyo naye alipaza sauti akiomba msaada kwa wananchi akidai anatekwa na watu ambao hawafahamu.
Shuhuda aliyezungumza na Mwananchi amesema baada ya kuona wananchi wanakimbilia eneo la tukio, alipiga simu polisi kuomba msaada kutuliza ghasia.
“Bada ya kuona hao watumishi wa TRA wamepiga simu polisi na hawajaja, niliwapigia na mimi na baada ya muda niliwafuata, kwa sababu tayari huyo dereva alishapiga kelele anatekwa watu waliendelea kukimbilia eneo la tukio wakiwa na mawe,” amesimulia shuhuda huyo.
Baada ya kufika kituoni na kutoa taarifa, shuhuda huyo ambaye ni dereva wa bodaboda amesema alipata mteja na kuondoka naye na hakurudi eneo la tukio kujua kinachoendelea.
Shuhuda mwingine ameeleza baada ya maofisa wale kuzungukwa na watu ambao walikuwa wakiwarushia mawe wakiwaita watekaji, walianza kuondoa gari lao kuokoa maisha.
“Hawakufika mbali waligonga kitu kwa mbele na vioo vya gari lao vilipasuliwa na baadaye polisi walifika kutuliza ghasia zile,” amesema.
Kamanda Muliro amewatahadharisha wananchi kuepuka kujichukilia sheria mkononi kwani watajikuta matatani.
“Wananchi watajiingiza kwenye matatizo, waache kujichukuliwa sheria mkononi,” ameonya Muliro.
Awali, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter ameandika: “Nimesikitishwa na tukio la kushambuliwa kwa watumishi watatu TRA na gari lao (STL 9923) walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kisheria ya kudhibiti magendo na magari yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria.”
Dk Mwigulu amewapa pole wote waliojeruhiwa na kuwaombea wapate nafuu haraka, akilaani tukio na kuahidi hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
“TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu wa sheria. Tunatoa wito kwa wananchi wote kushirikiana na Serikali kuhakikisha sheria za kodi zinatekelezwa ipasavyo kwa maendeleo ya Taifa letu. Tukumbuke, kodi zetu ndiyo maendeleo yetu,” amendika Dk Mwigulu.
Akizungumzia ukamataji unavyotakiwa kufanyika kisheria, ofisa mchechemuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Maduhu William amesema sheria zinazoeleza ukamataji ni pamoja na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, Kanuni za Kudumu za Polisi (PGP) na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
“Sheria hizo zinalipa mamlaka Jeshi la Polisi kumkamata mtu yeyote,” amesema.
Ametaja aina mbili za ukamataji ambazo ni wa kawaida unaofanyika mchana na wa usiku kuanzia saa tano.
“Kwa ukamataji wa mchana, polisi kwanza anatakiwa ajitambulishe na atoe kitambulisho. Amwambie anayemkamata kwamba yuko chini ya ulinzi kwa kosa fulani, kisha atampa nafasi awasiliane na ndugu zake ili wafike kumdhamini,” amesema.
Kuhusu ukamataji wa usiku amesema: “Askari anatakiwa awe na arrest warrant (hati ya ukamataji) kutoka kwa ofisa aliyemwagiza, anaweza kuwa kamanda wa polisi wilaya au mkoa. Pia anatakiwa aongozane na mashahidi, akiwemo mwenyekiti wa mitaa.”
Mbali ya ukamataji, Maduhu amesema kuna upekuzi, ambao askari atapaswa kuwa na hati ya ukaguzi na awe na mashahidi, akiwemo mwenyekiti wa mitaa.
“Mtuhumiwa atapata fursa ya kumkagua polisi ili asije kuwa na kitu ambacho anaweza kumbambika. Baada ya kufanya ukaguzi, polisi atajaza fomu (seizure form) kuonyesha vitu alivyokamata au alivyoondoka navyo na yule mtuhumiwa atasaini hiyo fomu.
“Ukamataji na upekuzi wowote ambao haufuati utaratibu huu unakuwa ni makosa kisheria, na ndiyo maana mahakama za juu huwa zinawaachia huru washitakiwa wanaokata rufaa kwa sababu ukamataji haukufuata utaratibu,” amesema.
Kuhusu askari wanaofanya doria usiku, amesema wanatakiwa kujaza movement order (hati ya kusafiri) na itasema hawataruhusiwa kuvuka maeneo wanayofanyia kazi.
“Huwa wanafanya doria kwa minajili ya kuimarisha ulinzi, lakini ikitokea uhalifu watatumia movement order kukamata,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwa baadhi ya maofisa wa polisi kuanzia cheo cha mrakibu wanaruhusiwa kukamata watu usiku bila hati ya ukamataji.
Kuhusu sare, amesema kuna askari wa aina mbili ambao ni wa kawaida na askari kanzu.
“Wale wa kawaida lazima wavae sare, lakini hawa makachero wanaweza kukamata bila sare, lakini ni lazima waonyeshe vitambulisho,” amesema.
Kuhusu mamlaka nyingine zinazofanya operesheni, amesema zinapaswa kuongozana na polisi wanapokuwa kwenye operesheni hizo.
“Hiyo pia ni kwa usalama wao kwa sababu zikitokea vurugu, wananchi wakiona polisi wanaamini kwamba hao ni watu wema.
“Pia sheria ya TRA inasema, maofisa wao wakitaka kukamata ni lazima wapate amri ya Mahakama. Kwa hiyo turudi kwenye sheria, haya yote hayatatokea,” amesema.
Mwanasheria, Hekima Mwasipu amesema maofisa wa TRA wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura namba 438 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Amesema ofisa wa TRA anaruhusiwa kufanya upekuzi na kukamata mali au mtu.
“Katika mazingira hayo, ni wakati gani anaruhusiwa na anatakiwa kuwa na nani. Kifungu namba 64 cha sheria ya usimamizi wa kodi, kinaeleza ofisa kodi wa TRA anatakiwa kuomba kibali cha mahakama ili kukamata mali, lakini lazima aeleze sababu, ingawa kosa limeshajulikana.
“Amri ya mahakama itasema ofisa kodi aambatane na ofisa wa Jeshi la Polisi kwa ajili ya ukamataji wa mali au gari imekwepa kodi,” anasema.
Mwasipu amesema sheria hiyo haijazungumza popote muda wa ukamataji, lakini Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022, inaeleleza masuala yote ya upelelezi na ukamataji wa sheria zozote au makosa yoyote nchini, sheria mama ndiyo itakayotumika ili ukamataji ufuate misingi ya kisheria.
“Sasa kwa kuwa sheria ya kodi ipo kimya tutakwenda kutumia sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, ambayo kama mtu anataka kukamata lazima aombe kibali cha mahakama kitakachomruhusu kukamata kuanzia saa 12 jioni na kuendelea.
“Ikitokea ukamataji huo umefanyika usiku bila kibali cha mahakama, basi ni batili,” amesema.
Kabla ya mtu kukamatwa na polisi, amesema lazima ajitambulishe kwa mhusika, cheo chake, anatokea kituo gani cha polisi.
“Akishajitambulisha kwako akuambie sababu za kukukamata, hizi ni haki za msingi. Haya yasipofanyika huu utakuwa ni utekaji, kwa sababu sheria zimeeleza wazi haki za mtuhumiwa, anayetaka kukamatwa na Jeshi la Polisi.
“Ifike hatua kwa mambo yanayoendelea sasa, Jeshi la Polisi, wanasheria watoe elimu kwa umma kuhusu wajibu wao pale wanapotaka kukamatwa,” amesema.