Spika Tulia aagiza vitabu vya mtaala mpya kufika mapema shuleni

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameagiza Serikali kuhakikisha vitabu vya mtaala mpya kwa shule za msingi ulioanza kutekelezwa, vinafika mapema kwa sababu wanafunzi wanafanya mitihani iliyo sawa.

Dk Tulia ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 9, 2024 baada ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga kujibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline Andrew.

Jacqueline Andrew amehoji nini mpango wa Serikali kuwezesha upatikanaji wa vitabu kwa shule za msingi ambazo zimeanza mtaala mpya wa Kiingereza kuanzia darasa la kwanza.

Akijibu swali hilo, Kipanga amesema ili kufanikisha hilo, Serikali imechapa na kusambaza nakala milioni 9.81 za mihtasari, vitabu vya kiada na kiongozi cha mwalimu kwa mchanganuo wa nakala 509,582 za mihtasari na mtaala ulioboreshwa wa elimu ya awali, msingi na sekondari.

Pia, amesema nakala milioni 8.06 za vitabu vya kiada vya kimacho (maandishi ya kawaida) kwa darasa la awali, darasa la I na la III kwa shule zinazotumia Kiswahili na Kiingereza kama lugha za kufundishia.

Amesema nakala 43,785 za vitabu vya maandishi yaliyokuzwa, nakala 6,990 za vitabu vya breli na nakala milioni 1.18 za viongozi vya mwalimu.

Amesema vitabu hivi vimesambazwa kwa uwiano kati ya 1:2 hadi 1:4.

Katika swali la nyongeza, Jacqueline amesema vitabu ambavyo havijasambazwa ni asilimia tisa na kuhoji Serikali imejipangaje kumalizia kiasi hicho kilichobaki.

Pia, amesema kutokana na jiografia ya Mkoa  wa Tabora ambao ni  mkubwa, Serikali imejipangaje kuhakikisha unapata kipaumbele kwenye usambazaji wa vitabu.

Akijibu swali hilo, Kipanga amekiri ni kweli kwa baadhi ya mikoa usambazaji wa vitabu hivyo haujafikia asilimia 100.

Ameitaja mikoa hiyo ni Iringa, Katavi, Mbeya, Mara, Mwanza Rukwa, Shinyanga, Simiyu,  Songwe na Tabora.

“Nimuondoe hofu mheshimiwa mbunge upelekaji wa vitabu hivi asilimia tisa iliyosalia unaendelea na hadi kufikia mwisho wa mwezi huu tutakuwa tumekamilisha kwa asilimia 100,” amesema.

Kuhusu kipaumbele kwa Mkoa wa Tabora, Kipanga amesema wanatarajia mwishoni mwa Mei mwaka huu, vitabu vyote vitakuwa vimefika katika mikoa yote.

Baadha ya majibu hayo, Dk Tulia aliitaka Serikali kuhakikisha vitabu hivyo vinafika mapema kwa sababu watoto watafanya mitihani inayofanana bila kujali wamepata kwa muda ama wamechelewa.

“Ni muhimu kulipa kipaumbele hiaki jambo, kama ulivyosema mwanzoni mwa Juni watoto wote wawe wamepata hivi vitabu,”amesema.

Related Posts