Mwili wa mchungaji aliyesubiriwa kufufuka kwa miezi miwili wazikwa

Iringa. Mchungaji wa Kanisa la El-Huruma (E.H.C), John Chida, ambaye mwili wake ulihifadhiwa ndani ya nyumba kwa miezi miwili tangu alipofariki dunia ikisubiriwa kuwa angefufuka, umezikwa.

Mwili wa Chida (47), umezikwa leo Desemba 6, 2024 katika makaburi ya Mlolo, Manispaa ya Iringa baada ya ndugu zake kupata taarifa kupitia vyombo vya habari.

Mwili wa mchungaji huyo anayeelezwa kufariki dunia Oktoba, 2024 uligunduliwa Desemba 3, ndani ya nyumba yake ukiwa umeharibika.

Muumini wa kanisa hilo, Agnes Mwakijale, anashikiliwa na polisi mkoani Iringa ikidaiwa alikuwa akiishi ndani na mwili wa mchungaji huyo akiamini angefufuka.

Ibada ya mazishi ya Chida imeongozwa na Mchungaji Godfrey Hezron wa Kanisa la ATCS Fellowship ambaye amesema hawawezi kufumbia macho matukio kama hayo.

Ruti Chida, mtoto wa marehemu amesema alipata taarifa kuhusu tukio hilo kupitia kwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isakalilo C, Amos Msole, kuwa baba yake amefariki tangu Oktoba.

Amesema alisafiri jana Novemba 5, usiku akitoka Dar es Salaam kwa ajili ya kumzika baba yake.

“Nilipata taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji imeniuma sana,ā€ amesema.

Job Chida, mdogo wa mchungaji huyo amesema familia imesikitishwa na kifo hicho, wakishangwa kwa sababu hawakutarajia hilo kutokea.

“Taarifa ya msiba tumeipata kupitia vyombo vya habari, tumefika usiku kwa ajili ya kumpumzisha ndugu yetu katika makaburi ya Mlolo,” amesema.

Ameishukuru Serikali kupitia mwenyekiti wa kitongoji cha Isakalilo ā€˜Cā€™ na Jeshi la Polisi kwa kuwa nao bega kwa bega katika msiba huo.

Chida alizaliwa mwaka 1977 mjini Kongwa mkoani Dodoma.

Imeelezwa katika wasifu wake kwamba alioa na kuzaa watoto wanne, wa kike wawili na wa kiume wawili.

Alihamia mkoani Iringa katika kujitafutia kipato na alikuwa mchungaji wa kanisa hilo lililopo Kitongoji Isakalilo C, Kata ya Kalenga wilayani Iringa.

Related Posts