Puma Energy yazindua kituo cha kwanza cha mafuta Z’bar

 

PUMA Energy Tanzania imezindua kituo cha kwanza cha kuuza mafuta ya gari na huduma za ziada katika eneo la Fuoni visiwani Zanzibar kwa lengo la kusogeza huduma za nishati ya mafuta karibu na wananchi sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Zanzibar katika uwekezaji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza leo tarehe 6 Desemba, 2024, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar Shaib Hassan Kaduara amesema wanapongeza kuzinduliwa kwa kituo hicho ambacho kinakwenda kusogeza huduma ya nishati ya mafuta na huduma za ziada kwa wananchi wa Zanzibar.

“Kituo hiki kipya cha Puma Energy Tanzania kitatumika kama kielelezo cha uwekezaji kwa siku nyingi zijazo zikionesha uwezo na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kuchochea ukuaji wa maendeleo ya shughuli za kijamii na kiuchumi hapa Zanzibar

“Nawashukuru Puma Energy Tanzania kwa uthubutu wao wa kuanza kutoa huduma ya mafuta kwa wananchi na hatua hii inakwenda kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati zenye bei nafuu na bora.

Kuzinduliwa kwa kituo hicho cha Mafuta cha Puma Energy Tanzania kinaendana na ajenda ya kukuza maendeleo ya usawa na kuboresha maisha ya wananchi wote wa Zanzibar .

Waziri Kaduara amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuwa mshirika wa Puma Energy Tanzania wakati wote na kuongeza siku zote wamekuwa tayari kutathimini fursa na mipango mipya ya kuwahudumia wananchi katika sekta ya nishati.

Pia amesema hatua hiyo ya Puma Energy Tanzania kuzindua kituo hicho cha mafuta inaashiria hatua nyingine ya maendeleo ya sekta ya nishati Zanzibar na ni uthibitisho wa ushirikiano wenye kuleta tija kati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi kama Puma Energy Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo imekuwepo Zanzibar tangu mwaka 1994 na wanatoa huduma ya nishati ya mafuta ya ndege lakini sasa wanazindua kituo chao cha kwanza cha kuuza mafuta ya magari na vyombo vingine vya moto.

Ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji visiwani humo na kuongeza uchumi wa Zanzibar unakuwa sana na kuongeza Puma Energy Tanzania wataendelea kuzindua vituo vya mafuta Unguja na Pemba na hiyo ni dhamira yao kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar.

Kuhusu kituo hicho, Mkurugenzi Mtendaji Fatma Abdallah amesema kimetumia zaidi ya Sh. 25 bilioni hadi kukamilika kwake na kimetoa ajira kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya Fuoni na kusisitiza kituo hicho kitatoa huduma katika Viwango vya Kimataifa.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Tanzania Dk. Selemani Majige amesema Kampuni hiyo inajivunia ubora wa bidhaa zake na kuongeza mkakati wao kwa Zanzibar ni kuendelea kusogeza huduma zake visiwani Zanzibar.

Pia amewaomba wananchi wa Zanzibar kuendelea kuungana katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa pande zote mbili za muungano za Tanzania Bara na Zanzibar.

About The Author

Related Posts