SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR YAIPONGEZA PUMA ENERGY TANZANIA KUZINDUA KITUO CHA MAFUTA NA HUDUMA ZA ZIADA

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Maji,Nishati na Madini katika Serikali ya Zanzibar Shaib Hassan Kaduara ameipongeza Puma Energy Tanzania kusogeza huduma ya nishati ya mafuta na huduma za ziada kwa wananchi wa Zanzibar baada ya kuzindua kituo cha kuuza mafuta Unguja visiwani Zanzibar.

Puma Energy Tanzania imezindua kituo hicho ambacho ni cha kwanza katika visiwani vya Zanzibar na lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya nishati ya mafuta ya gari karibu na maeneo yao sambamba na kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar katika kufungua uchumi na kuleta maendeleo.

Waziri Kaduara aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo ambao pia ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Puma Energy Tanzania Dr. Selemani Majige na Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah, amesema kituo hicho cha mafuta kimezinduliwa wakati sahihi kwani sera ya Serikali ni kusogeza huduma za nishati kwa wananchi.

Ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuwa mshirika wa Puma Energy Tanzania wakati wote na kuongeza siku zote wamekuwa tayari kutathimini fursa na mipango mipya ya kuwahudumia wananchi katika sekta ya nishati.

Amesisitiza hatua hiyo ya Puma Energy Tanzania kuzindua kituo hicho cha mafuta inaashiria hatua nyingine ya maendeleo ya sekta ya nishati Zanzibar na ni uthibitisho wa ushirikiano wenye kuleta tija kati ya Serikali na wadau wa sekta binafsi kama Puma Energy Tanzania .

Akieleza zaidi amesema kituo cha mafuta cha Puma Energy Tanzania katika visiwa hivyo kitatumika kama kielelezo cha uwekezaji kwa siku zijazo zikionesha uwezo na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi katika kuchochea ukuaji wa maendeleo ya shughuli za kijamii na kiuchumi hapa Zanzibar

“Nawashukuru Puma Energy Tanzania kwa uthubutu wao wa kuanza kutoa huduma ya mafuta kwa wananchi na hatua hii inakwenda kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati zenye bei nafuu na bora.Kuzinduliwa kwa kituo hicho cha Mafuta cha Puma Energy Tanzania kinaendana na ajenda ya kukuza maendeleo ya usawa na kuboresha maisha ya wananchi wote wa Zanzibar .

Awali akizungumza kuhusu kituo hicho cha mafuta ambacho ni cha kwanza Zanzibar,Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa huduma Zanzibar tangu mwaka 1994 na wakati wote huo wamekuwa wakitoa huduma ya kuuza mafuta ya ndege na sasa wamezindua kituo cha mafuta kwa ajili ya vyombo vya moto yakiwemo magari.

“Tunatoa shukrani kwa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuongeza uchumi wa Zanzibar kwa kuhakikisha unaendelea kukua kwa kasi.Kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji Puma Energy Tanzania dhamira yetu ni kuendelea kuongeza vituo mafuta Unguja na kwa Pemba tunatarajia ifikapo mwaka 2025 tuwe na kituo cha mafuta.”

Mkurugenzi Mtendaji Fatma Abdallah amesema kimetumia zaidi ya Sh.bilioni 2.5 hadi kukamilika kwake na kimetoa ajira kwa wananchi wanaozunguka.maeneo ya Fuoni na kusisitiza kituo hicho kitatoa huduma katika Viwango vya Kimataifa.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy Tanzania Dk.Selemani Majige amesema Kampuni hiyo inajivunia ubora wa bidhaa zake na kuongeza mkakati wao kwa Zanzibar ni kuendelea kusogeza huduma zake visiwani Zanzibar.

Pia amewaomba wananchi wa Zanzibar kuendelea kuungana katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo kwa pande zote mbili za muungano za Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tunawaomba wananchi wa Zanzibar kuja katika kituo hiki kununua mafuta ambayo ni bora na mkakati wetu Puma Energy Tanzania ni kuendelea kusogeza huduma na bidhaa zetu kwa wananchi.”





Related Posts