Watu 237 wapanda Mlima Kilimanjaro kusherehekea Uhuru

Moshi. Watu 237, wakiwemo mabalozi tisa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani, wameanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.

Safari hiyo ya kupanda mlima inaongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) chini ya Kanali Deus Babuu na itachukua siku tano kupitia njia ya Marangu.

Watu hao wanatarajiwa kufika kilele cha mlima huo, maarufu kama Uhuru Peak, tarehe Desemba 9, 2024, kusimika bendera ya Taifa katika kilele hicho, na kushuka tarehe Desemba 10, 2024.

Akizungumza wakati wa kuwaaga wapanda mlima hao, Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lazaro Twange, amesema kuwa moja ya kazi muhimu za mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi ni kutangaza vivutio na mazuri yaliyopo nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji na watalii.

Twange, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesisitiza kuwa ni jukumu la Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na wadau wengine wa utalii nchini kuhakikisha mazingira ya utalii yanakuwa bora kwa kuondoa urasimu wa barabarani na kuzuia usumbufu kwa watalii.

“Shughuli hii ya mabalozi kupanda Mlima Kilimanjaro ina heshima ya kipekee, kwani wanatangaza mazuri ya nchi yetu na kuhamasisha watu kuja Tanzania. Hivyo, sisi tulioko nyumbani tunatakiwa kuhakikisha tunapunguza maswali ambayo mabalozi hao wanaweza kukutana nayo nje wanapovutia watu kuja nchini,” alisema Twange.

Ameongeza kuwa ni muhimu mazingira yanayokuta wageni yafanane na yale wanayoambiwa kabla ya kuja.

“Mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa na wadau wengine, tuendelee kulinda na kuboresha mazingira ya utalii ili mabalozi na wageni wetu wakija wakute mazingira mazuri,” alisema Twange.

Aidha, aliwahimiza wadau wa utalii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Tanapa, Jenerali Mstaafu George Waitara, amewasihi wapanda mlima hao kuzingatia maelekezo ya waongoza watalii na kuepuka mashindano ya haraka katika kupanda mlima.

“Mabalozi, naamini mtafika kileleni. Mlima huu unaheshimika na unahitaji uvumilivu. Fuata maelekezo ya waongoza watalii, tembea polepole, na mshirikiane kama timu. Ikiwa mtafuata taratibu, mlima huu utakuheshimu,” alisema Waitara.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa Tanapa, Massana Mwishawa, amesema kuwa watu 300 wanapanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia tatu tofauti kwa maadhimisho hayo ya uhuru.

Kundi la kwanza lilianza safari tarehe 3 Desemba 2024 kupitia njia ya Lemosho, likifuatiwa na kundi la pili tarehe 4 Desemba kupitia njia ya Machame. Kundi la tatu, ambalo ni kubwa zaidi, linapitia njia ya Marangu na limeandaliwa na kampuni ya utalii ya Zara.

“Tunaamini kupitia mabalozi hawa na wengine wanaoshiriki, Tanzania itapata wageni wengi zaidi kutoka nchi wanazoziwakilisha,” amesema Mwishawa.

Related Posts