Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Baraza la Watumiaji wa Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA CCC), Innocent Kyara amesema katika kuadhimisha miaka 80 ya usafiri wa anga, haki za abiria na watumiaji wa sekta hiyo zinapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza.
TCAA CCC ni taasisi ya Serikali kwa ajili ya kumlinda, kumtetea na kumwakilisha mtumiaji wa usafiri wa anga nchini.
Kyara amesema hayo leo Ijumaa Desemba 6, 2024 akichangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi X-Space (zamani twitter) uliondaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na TCAA ukijadili maadhimisho ya miaka 80 ya usafiri wa anga duniani.
“Matumaini yetu ni kuwa, masuala yote ya uamuzi na uendeshaji wa sekta ya anga yanamuangalia mtumiaji na mahitaji yake kwanza.
“Unataka kufanya jambo lolote iwe ni Serikali, TCAA au watoa huduma za anga swali wanalopaswa kujiuliza, ni jambo hili ninalotaka kulifanya litaleta athari gani kwa mtumiaji, iwe hasi au chanya,” amesema.
Amesema watumiaji ndiyo wanaibeba sekta ya anga na kwamba, mambo mengi yanayofanyika yanalinda watoa huduma kwa gharama za mtumiaji ili kuleta uhimilivu wa sekta hiyo.
Ameyataka mashirika ya ndege kuboresha huduma zake pindi ndege zinapochelewa au safari kuahirishwa, ikiwemo malipo ya fidia.
“Ikitokea safari imeahirishwa kunastahili malipo ya fidia, endapo ikathibitishwa safari imefutwa au kuahirishwa kumemletea hasara.
“Lakini taarifa sahihi zinazojitosheleza zitoke mapema kama ndege haitaondoka kwa muda uliopangwa, katika nchi zilizoendelea malipo ya fidia utaona wanakutumia ujumbe wa kuombwa radhi kuhusu ndege kuchelewa, wanakwambia kulingana na taratibu unatakiwa kulipwa fidia,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TCAA, Maria Memba, amesema chochote kinachoonekana katika sekta ya usafiri wa anga kina kanuni zake, hivyo kitakachoonekana ni hatarishi kimewekewa kanuni.
Amesema kuna sheria ambazo abiria anatakiwa kufuata endapo hajaridhishwa na usafiri wa anga kwa maana ya kuachwa na ndege, amecheleweshewa mzigo au amepata ajali kwenye ndege. Ameeleza kuna kanuni zimeweka viwango mbalimbali vinavyotakiwa kulipwa kwa mtu aliyeathiriwa.
“Na sisi tuna kitengo chetu ambacho kinasikiliza malalamiko ya abiria wa aina hiyo, kwa yeyote ambaye ameathirika na huduma ya anga kanuni zinamtaka afike katika mamlaka popote alipo kwa kujaza fomu na sisi tunaangalia kama malalamiko yana ukweli, ” amesema.
Amesema kumekuwa na mwamko kwa siku za hivi karibuni, akieleza wanaweza kupokea malamiko hata 10. Amesema hilo linatokana na jitihada wanazoendelea kuchukua kwa kutoa elimu kuhusu haki za abiria.
Mbali ya hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi amesema sekta hiyo inakua kwa kasi hivi sasa, akieleza katika mwaka wa fedha 2023/2024 walihudumia abiria milioni 6.8 katika viwanja vyote vilivyopo Tanzania.
Amesema katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, wanatarajia utakapokamilika watakuwa wamehudumia abiria milioni 7.5 kwa viwanja vyote vya ndege.
“Ukiangalia kitakwimu kasi yake ni kubwa, inaonyesha watumiaji wanaongezeka. Wanapoongezeka tusiwakatishe tamaa, tunatakiwa kuboresha huduma zetu kwa wale wanaotoa huduma viwanjani, mashirika ya ndege na watoa huduma za mizigo ili kuvutia abiria,” amesema.
“Huku tunakokwenda usafiri wa anga ili uwe endelevu lazima kuimarisha usalama,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma ya Anga Tanzania (TAOA), Mrisho Yassin amesema sekta hiyo ni pana na wapo watu wengi wanaoajiriwa, hivyo wanashiriki kutoa mafunzo kwa wanachama wao.
Amesema chama hicho kina wadau wengi, hivyo wanatoa mafunzo kwa marubani, mafundi, huduma kwa wateja na kuhusu mizigo hatarishi.
Amesema wanafanya biashara kwa kuwa kampuni zinalipa kodi, hivyo wapo makini katika utoaji huduma zikiwamo kwa sekta ya utalii.
“Watalii wanapokuja sisi ndio kioo cha kwanza, wanapozunguka katika nchi yetu wanatumia usafiri wa anga wa mashirika ya ndani kwa hiyo mchango wetu ni mkubwa,” amesema.