Mbeya. Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kimesema mradi wa Mageuzi ya Elimu kwa Maendeleo ya Uchumi (HEET), utasaidia kumaliza changamoto ya miundombinu inayokikabili chuo hicho.
Akizungumza leo Desemba 6 kwenye mahafali ya 12, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Aloys Mvuma amesema hadi sasa kuna uchache wa miundombinu, lakini mradi wa HEET unatarajiwa kumaliza changamoto hiyo.
Amesema chuo hicho kimekuwa na mafanikio mengi, ikiwa ni pamoja na udahili wa wanafunzi, kutoa mafunzo ya utafiti na ubunifu, mafunzo ya kitaaluma, na kwamba tayari wamesaini makubaliano na taasisi 10 zikiwemo za kimataifa katika nyanja ya elimu kuwaandaa wanafunzi kiushindani katika soko la ajira.
“Tunatarajia ujenzi wa majengo kukamilika Desemba mwaka huu kwani ujenzi wake upo asilimia 98, na Januari mwakani yaanze kutumika. Hali hii itasaidia kuongeza wigo wa chuo katika kudahili wanafunzi,” amesema Profesa Mvuma.
“Chuo kilitenga Sh180 milioni kwa ajili ya mafunzo mbalimbali ya ubunifu kwa kushirikiana na wadau katika hali ya kuwasaidia wanafunzi kujiweka kwenye soko la ushindani ndani na nje kwenye fursa za ajira,” ameongeza.
Mapema, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Zakia Meghji amesema hadi sasa utekelezwaji wa mradi wa HEET unaenda vyema, akiwataka wasimamizi kumaliza ujenzi kwa muda muafaka.
Amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia shughuli za ufundishaji, ujifunzaji, kuongeza idadi ya udahili, na kupanua mapato ya Chuo.
“Mradi huu unagharimu Sh73 bilioni ambapo utekelezaji wake unaenda vyema. Nisisitize wasimamizi kutobweteka na kumaliza kwa muda uliopangwa,” amesema Meghji.
Kwa upande wake, mdau wa chuo hicho, Dk Lulu Luflenge amewataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kutafuta fursa wenyewe na kuendelea kuwa mabalozi wa chuo hicho.
“Tunajivunia mafanikio mengi kwa kuwatoa viongozi wengi chuoni hapa. Tunatarajia kuona mkitumia elimu kuinufaisha jamii na kukuza maendeleo ya Taifa kwa kuchangamkia fursa bila kusubiri ajira,” amesema Dk Lulu.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, mwanafunzi bora wa chuo hicho, Ashiru Mussa amesema wamepata elimu ambayo itakuwa mkombozi kwao katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Ameshauri chuo hicho kuendelea kutengeneza fursa mbalimbali na kusimamia misingi ya elimu bora kwa ajili ya ustawi wa Taifa katika teknolojia.
“Tunaamini elimu hii itatuongoza katika maisha yetu kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Tunapongeza uongozi kwa misingi bora iliyotujenga, na tunaomba mikakati hii iwe endelevu,” amesema Mussa, muhitimu wa ngazi ya Shahada ya Uhandisi wa Vifaa Tiba.