Gharama kubwa za masomo chanzo upungufu wa marubani

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, amesema Tanzania inakabiliwa na uhaba wa marubani zaidi ya 150, licha ya juhudi zinazoendelea za kuongeza idadi yao nchini.

Amesema changamoto kubwa iliyopo ni gharama kubwa ya mafunzo, ambapo kumwandaa rubani mmoja hadi kufikia kiwango cha kuendesha ndege kunagharimu takriban Sh200 milioni.

Ili kupunguza mzigo huu na kuimarisha sekta ya usafiri wa anga, Msangi amesisitiza umuhimu wa kuwa na vyuo vya mafunzo vya ndani, ambavyo vitazalisha marubani wa kutosha, si tu kwa ajili ya mahitaji ya ndani bali pia kwa ajili ya soko la kimataifa.

“Mamlaka jukumu letu ni kuhakikisha vyuo vinakuwa vingi, tunavisajili nchini kwa hiyo ni sehemu ya kuleta wawekezaji ambao watawekeza kwenye vyuo hivi na kupata marubani wa kutosha,” amesema.

Amesema hayo leo Ijumaa Desemba 6, 2024 akichangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi X-Space (zamani twitter), uliondaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ukijadili maadhimisho ya miaka 80 ya usafiri wa anga duniani.

Awali, Mhariri, Dawati la Uchumi wa gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema usafiri wa anga ni miongoni mwa sekta muhimu za kiuchumi kwa watumiaji na wasioutumia huduma hiyo moja kwa moja, lakini unawanufaisha.

Amesema sekta hiyo ndiyo usafiri wa haraka hivi sasa kuliko mwingine wa kuwezesha watu kutoka eneo moja kwenda jingine. Amesema usafiri wa anga pia unasafirisha mizigo haraka, hivyo unabaki kuwa kiungo muhimu katika uchumi.

“Usafiri wa anga ni miongoni mwa sekta zilizofungamanishwa kwa ukaribu na sekta za utalii. Kwa sehemu kubwa utalii unachangiwa na uwepo wa huduma za usafiri wa anga. Mtu anaweza kutoka Uingereza, kesho yupo Kilimanjaro, au Seoul (Korea) akaja Tanzania kwa urahisi,” amesema.

Amesema takribani watu bilioni 10 duniani wanatumia usafiri huo, huku mtu mmoja anaweza kuutumia hata mara 10 kwa mwaka na mwingine mara moja.

Amesema sekta ya usafiri wa anga imetoa ajira kwa watu kutoa huduma ndani ya ndege, au kampuni zinazoshughulikia mizigo na wengine wameajiriwa na mashiriki ya ndege kwa kazi zisizo za moja kwa moja.

“Kwa sehemu kubwa shughuli za usafiri wa anga zinatumika zaidi kukuza au kuimarisha sekta zingine, ikiwemo kufanikisha mikutano ya kibiashara. Usafiri wa anga unakuwa na usalama wa uhakika zaidi, kuliko magari, yote hayo yanaonyesha sekta hii ni muhimu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Msangi amewataka waingizaji na watumiaji wa ndege zisizo na rubani (drones) kuzingatia na kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali kuhusu matumizi yake.

Amesema kuleta drones nchini haikatazwi, kichotakiwa ni kufuata utaratibu ikiwemo kupata kibali, kuisajili na wakati wa kuitumia upate kibali cha matumizi.

“Unapokamatwa, angalia sheria imeanisha adhabu, kwamba unapoitumia utaadhibiwa kwa kiasi gani, tusingependa watu waingie kwenye mgogoro wa kisheria ila watumie kwa utaratibu wa kisheria.

“Siyo pesa nyingi iliyowekwa, bali ni kuhakikisha tunadhibiti vyombo hivi visiingiliane na ndege zingine zinazotumia anga na kusababisha ajali,” amesema.

Amesema wapo wanaoingiza drones kupitia maeneo yasiyo rasmi au uwanja wa ndege kwa njia ya ujanja, hata hivyo zikiingia nchini lazima zisajiliwe, na huwezi kufanya hivyo pasipo kueleza namna ulivyoiingiza.

“Hivi karibu tumekaa na vyombo vya ulinzi na usalama, tutaanza kuwasaka wale wote waliongiza drones kinyemela ili sheria ifuate mkondo wake. Wale walioingiza kwa kufuata utaratibu wahakikishe wanapata kibali wakitaka kuzitumia.

“Kuna wengine waliingiza drones kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Amani (Abeid Amani Karume) na wa Julius Nyerere, zitakamatwa kwa sababu hawakuomba kibali cha kuingiza. Ukiingia nayo na ikigundulika itazuiwa, utaruhusiwa kuondoka na kutafuta kibali cha kuingiza drones nchini, usipofuatilia utakuwa umeitelekeza,” amesema.

Msangi amesema kuna wengine walikamatwa wakizitumia na sheria ilifuata mkondo wake, ndiyo maana amewataka watu kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.

Related Posts