Kesi ya jaribio la kumteka Tarimo kuanza kuunguruma Desemba 19

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni iliyoko Kinondoni imepanga kuanza kusikiliza kesi ya jaribio la utekaji wa mfanyabiashara Deogratius Tarimo kuanzia Desemba 19, 2024.

Mahakama hiyo imepanga tarehe hiyo kuanza kusikiliza kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kuieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Washtakiwa katika kesi hiyo wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka linalowakabili leo Ijumaa, Desemba 6, 2024.

Washtakiwa ni Fredrick Juma Said mjasiriamali, Isack Mwaifani, Benki Mwakalebela ambaye ni wakala Stendi ya Magufuli,  Bato Bahati Tweve, Nelson Elimusa ambaye  dereva wa teksi na Anita Temba.

Wote kwa pamoja wanaokabiliwa na shtaka moja la kujaribu kuteka mtu na kumuweka kizuizini isivyo halali kinyume na vifungu vya 380(1) na 381(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Akiwasomea shtaka hilo, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali John Mwakifuna amesema kuwa Novemba 11, 2024, katika eneo la Kiluvya Madukani Lingwenye, jijini Dar es Salaam walijaribu kumteka mfanyabiashara Deogratius Tarimo kwa nia ya kumuweka kizuizini isivyo halali.

Washtakiwa wote wamekana shtaka hilo na Wakili Mwakifuna ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na akaomba Mahakama ipange tarehe kwa ajili ya usikilizwaji awa awali.

Washtakiwa wote, ambao hawakuwa na uwakilishi isipokuwa Nelson ambaye amewakilishwa na Wakili Nestory Wandiba, wameomba dhamana na Wakili Mwakifuna amesema kuwa hana pingamizi kwa kuwa shtaka lao linadhaminika.

Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira anayesikiliza kesi hiyo amewaeleza washtakiwa kuwa dhamana yao iko wazi kwa masharti ya kusaini bondi ya dhamana ya Sh10 milioni kila mmoja.

Masharti mengine ya dhamana ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka kwa waajiri wao kama ni waajiriwa, au kutoka Mtendaji wa Kata.

Pia hawatakiwi kutoka nje ya Mkoa bila ruhusa ya Mahakama.

Hakimu Rugemalira ameahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 19, 2024 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali na usikilizwaji kamili, ambapo washtakiwa watasomewa maelezo ya awali na kisha Mahakama itaanza kupokea ushahidi kutoka kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Hakimu Rugemalira ameamuru washtakiwa kupelekwa mahabusu mpaka tarehe hiyo, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Related Posts