Diarra, Camara watungiwa sheria mpya Fifa

BODI ya Kimataifa ya Vyama vya Soka (IFAB) inayojihusisha na utungaji wa sheria kwenye mchezo wa soka imefichua kwamba kuna jambo jipya linakuja hivipunde kwenye soka la dunia.

Ni jambo ambalo huenda likawa na faida kubwa kwa mashabiki haswa wa Ligi za Afrika na nchi zingine zinazoendelea kwani watapata muda mwingi wa kuinjoyi soka kuliko ilivyo sasa ambapo kuna baadhi ya mambo yanawafanya wakose ladha.

Makipa mbalimbali maarufu duniani wakiwemo Djigui Diarra wa Yanga na Mousa Camara, waliozowea kudaka kisha kulala na mpira kupoteza muda watakumbana na adhabu endapo tu itazidi sekunde nane kama muswada mpya utapitishwa na kuwa sheria mpya kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

IFAB imefichua kwamba kwenye sheria hiyo mpya waamuzi watamwaadhibu atakayekumbatia mpira muda mrefu kuzidi uliopangwa basi timu pinzani itapewa faida ya pigo la mpira wa kona.

Kwa mujibu wa The Times la Uingereza, sheria hiyo mpya itawataka waamuzi kuhesabu sekunde kwenye saa zao kwa kuanzia sekunde tano kushuka chini hadi sifuri na baada ya hapo atampa ishara kipa aliyeng’ang’ania mpira kwa muda mrefu kwamba inapaswa kupigwa kona kwenye goli lake.

Sheria hiyo inaletwa ili kuwadhibiti makipa wenye tabia za kupoteza muda na sasa ipo kwenye majaribio huko Malta, Ligi Kuu England kwa timu za chini ya umri wa miaka 21 na kwenye mashindano ya vijana huko Italia.

Sheria ya sasa ni kwamba makipa wamekuwa wakionyeshwa kadi za njano kama mwamuzi akiona kwamba amechelewesha mchezo kwa makusudi. Na waamuzi wa nguvu pia ya kuamuru ipigwe pigo lisilokuwa la moja kwa moja (indirect free kick) endapo kama kipa atakaa kwa muda mrefu na mpira kwenye mikono yake.

Hata hivyo, jambo hilo limekuwa nadra kutokea kwasababu ya muda zaidi kuongezwa ili mabeki wapata nafasi ya kujipanga kwenye nafasi zao. Lakini, pia ingetoa nafasi ya wapinzani kupata fursa ya kufunga bao rahisi.

Patrick Nelson, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Soka cha Ireland na mjumbe wa bodi ya IFAB, alisema: “Takwimu zilizopatikana kwenye majaribio zinavutia. Majaribio mawili yaliyofanyika yalikwenda vizuri na kipa aliyekaa na mpira muda mrefu, mwamuzi aliamuru ipigwe kona dhidi yao. Hiyo itasaidia makipa sasa kuharakisha kuachia mpira ili mchezo uendelee.”

Kwenye majaribio yaliyofanyika Malta imeelezwa kwamba adhabu ya mpira wa kurushwa badala ya kona iliyolewa kwa timu ambayo kipa wa upinzani alikaa na mpira kwenye mikono yake kwa muda unaozidi sekunde nane. Makipa walikuwa na mpira kwenye mikono yao mara 796 na hakuna aliyezidisha sekunde nane.

Nelson aliongeza: “Huu ni mtego kwa makocha na kipa yeyote ambaye atakaa na mpira muda mrefu akasababisha ipigwe kona au mpira wa kurushwa kwenye goli lake na kisha kusababisha timu ifungwe, kila huyo hatafanya hivyo mara mbili. Hii itakwenda kubadili tabia za makipa.”

Wakati huo huo, IFAB ina mpango pia wa kubadili sheria ya kuotea baada ya pendekezo la kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger, ambaye kwa sasa ni bosi wa Fifa anayesimamia maendeleo ya mchezo wa soka duniani. Sheria mpya kuotea inataka mchezaji wa timu pinzani anayeshambulia awe amezidi mwili mzima kutoka kwa beki wa mwisho na si ilivyo sasa, kuzidi kiungo tu. Kama mwili wa mchezaji anayeshambulia utakuwa umezidi beki wa mwisho, lakini kiungo chake kimoja kama mguu ukiwa sawa na mchezaji huyo wa mwisho, hiyo haiwezi kuhesabika kama tukio la kuotea.

Mkurugenzi wa ufundi wa IFAB, David Elleray alisema: “Tunaendelea na majadiliano kuhusu mabadiliko haya.”

Sheria hiyo mpya itawaweka mtegoni makipa Djigui Diarra wa Yanga na Moussa Camara wa Simba endapo kama itapitishwa na kuletwa kwenye Bara la Afrika, ambapo wakali hao watazitumikia timu zao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho (CAF) mtawalia.

Related Posts