Fadlu kutumia mbinu hizi, kuimaliza CS Constantine 

SIMBA inaendelea kujifua ikiwa Algeria kwa ajili ya mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine utakaopigwa kesho kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mohamed-Hamlaoui nchini Algeria.

Wekundu hao ambao wamewahi kufuzu robo fainali mara tano kati ya sita waliyoshiriki mashinda ya klabu Afrika, wanashuka katika mchezo huo wa pili wa kundi A la mashindano hayo wakiwania kufuzu robo fainali katika mchezo unaotajwa kuwa mkali na wa kusisimua.

Lakini wakati ukittafakari mchezo huo elewa kwamba  Kocha Fadlu Davids amepanga kufungia wenyeji wao busta zote ili kuhakikisha kwamba anarejea Dar akiwa na pointi muhimu mikononi mwake.

Simba na Constantine zilizopo Kundi A kila moja ilishinda mechi ya kwanza na kujikusanyia pointi tatu kila moja na bao moja, Wekundu wakiinyoosha Kwa Mkapa Bravos do Maquis ya Angola 1-0 kama walivyoshinda Waalgeria dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia. 

Kwa kutambua ugumu wa pambano hilo na kiu ya kuondoka na pointi ugenini, Fadlu amesema hawatashuka kizembe uwanjani mbele ya wenyeji kwani wanahitaji kukusanya pointi za kuwapeleka mbele katika kundi hilo analolitaja kuwa ni gumu.

Kocha huyo anajivunia wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kuibeba timu hiyo inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa pia nduio timu iliyofunga mabao mengi (22)na kufungwa machache (matatu) katika mechi 11, akiwamo Jean Ahoua, Steven Mukwala, Leonel Ateba na Debora Mavambo.

Mbali na nyota hao wa eneo la mbele, lakini uwepo kipa Moussa Camara anayeiongoza kwa ‘clean sheet’ na mabeki wazoefu Shomary Kapombe, Hussein Mohammed ‘Tshabalala’, Fondoh Che Malone na wengine imemfanya Fadlu achekelee akiamini akijipanga vyema ataondoka japo na pointi moja ugenini.

“Kucheza ugenini ni tofauti na nyumbani, lakini tupo hapa kwa ajili ya kufanya kila ambacho tunaweza ili kupata pointi ambazo zitatuweka kwenye mazingira mazuri, wachezaji wangu wanaendelea vizuri na wanaonyesha kuwa tayari. Hatutakaa nyuma, tutacheza kwa nidhamu huku tukicheza soka letu,” amesema Fadlu na kuongeza:

“Tulipata muda wa kuwasoma wapinzani wetu, tunajua ubora walionao lakini muhimu zaidi nguvu zetu tumeweka katika maandalizi yetu na mpango ambao naamini unaweza kufanya kazi.”

Katika mchezo uliopita, Simba ilishinda bao 1-0 kwa  penalti kupitia Ahou anayeongoza kuhusika na mabao mengi Ligi Kuu akiwa na Wekundu wa Msimbazi akifunga matano na kuasisti manne hadi sasa.

Kwa upande wake, kocha wa CS Constantine, Kheireddine Madoui ameonyesha kuwa na pigo katika kikosi kutokana na kukosekana kwa wachezaji watatu muhimu wa kikosi cha kwanza kabla ya mchezo huo. 

Wachezaji hao ni kiungo mshambuliaji Abdennour Iheb Belhocini mwenye mabao mawili na asisti moja katika michezo 10 na kiungo mkabaji Salifou Tapsoba aliyetumika katika michezo sita na mshambuliaji mmoja, Mounder Temine. 

Akizungumzia hilo, Madoui amesema: “Tunapokosa wachezaji muhimu tunajua kuwa tutakutana na changamoto kubwa. Hii ni hali inayotufanya tuwe na wasiwasi, hasa kwa kuwa Tamine, Belhoussini na Tapsoba hawatakuwepo.”

“Tamine na Belhoussini hatutakuwa nao kutokana na majeraha na Tapsoba ameondoka kwa ajili ya majukumu ya kimataifa,” ameongeza Madoui na kusisitiza licha ya vikwazo hivyo anatarajia timu itapambana kwa nguvu ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Madoui alisema licha ya changamoto za kiufundi, timu yake ina morali ya kupambana.

“Simba ni timu inayoheshimiwa sana katika mashindano ya kimataifa kutokana na uzoefu wake, na tunahitaji kujiandaa kwa makini,” amesema kocha huyo.

“Hata hivyo, sare ya hivi karibuni dhidi ya Union Biskra imetufanya tujiamini (walitoka nyuma), na sasa tunajua kuwa mchezo huu ni muhimu zaidi. Pointi zake zitakuwa na umuhimu mkubwa kwa safari yetu ya kufika mbali katika michuano hii.”

Takwimu zinaonyesha katika michezo mitano iliyopita ya mashindano yote (nyumbani na ugenini), ikiwemo mmoja wa Kombe la Shirikisho, CS Constantine inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Algeria imeruhusu mabao matatu na kufunga matano, ikiwa na wastani wa kuruhusu mabao 0.6 na kufunga ni bao moja kila mchezo. 

Katika michezo hiyo mitano iliyopita, CS Constantine imeshinda mitatu, ukiwamo mmoja wa Shirikisho dhidi ya CS Sfaxien kwa bao 1-0, huku mingine ikiwa dhidi ya Olympique Akbou (2-1) na USM Alger (1-0) ya Ligi Kuu, yote ni kwa tofauti ya bao moja tu. Hivyo inaonyesha sio timu yenye uwezo mkubwa wa kufunga.

Ndani ya michezo mitano ya mwisho ikiwa nyumbani tu, CS Constantine imeruhusu bao katika michezo minne, ni mchezo mmoja tu ambao nyavu zao hazikugushwa ambao ni dhidi ya  USM Alger, kitu ambacho  kocha Fadlu anaweza kutumia udhaifu huo kuwa faida  kwa upande wake.

Wakati CS Constantine ikionekana kuwa ni timu inayofungika kulingana na takwimu za michezo yao mitano iliyopita, Simba inaonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao 10 katika michezo yake mitano iliyopita, wanawastani wa kufunga mabao mawili.

Tofauti na CS Constantine iliyopoteza na kutoa sare mara moja moja, Simba yenyewe imeshinda michezo mitano mfululizo, ikiwemo mmoja wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos na minne ya Ligi Kuu dhidi ya Namungo (3-0), Mashujaa (1-0), KMC (4-0) na Pamba (1-0). 

Mbali na Simba kuwa na safu kali ya ushambuliaji, imeonyesha kuwa na ngome imara ambayo imewafanya ndani ya michezo hiyo kutoruhusu bao, msimu huu Simba imeruhusu bao moja tu katika mashindano ya kimataifa na ilikuwa dhidi dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Ethiopia wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1 Uwanja wa Benjamini Mkapa na kutinga makundi kibabe.

Related Posts