‘Vifo magonjwa yasiyoambukiza vyapunguza umri wa kuishi’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imesema kasi ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza inazidi kuongezeka hali inayosababisha Watanzania wengi kushindwa kufikia umri wa miaka 66 ambao ni wastani wa kuishi.

Takwimu zinaonyesha vifo vingi vinasababishwa na magonjwa ya Shinikizo la juu la damu, saratani, kisukari, afya ya akili na ajali mbalimbali.

Akizungumza Desemba 6,2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upimaji magonjwa yasiyoambukiza Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk. Hamad Nyembea, amesema vifo saba kati ya 10 vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

Kampeni hiyo imeandaliwa na Chama cha Watumishi wa Afya waliopata mafunzo na ujuzi Korea Kusini – KOFIH Global Alumni (KGA) kama njia ya kurudisha ujuzi na maarifa yaliyopatikana kupitia mafunzo hayo.

“Magonjwa yasiyoambukiza ni janga ambalo linazidi kuongezeka, kwa siku za karibuni na zijazo yataendelea kuwa chanzo cha vifo vya mapema…wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania ni kati ya miaka 64 hadi 66 lakini wengi hawafiki kutokana na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Dk Nyembea.

Aidha amesema kila mwaka kunaripotiwa visa vipya vya saratani 45,000 na vifo 30,000 sawa na asilimia 33 ya vifo vyote nchini na kila kifo kimoja katika vifo vitatu kinatokana na saratani.

Mkurugenzi huyo amesema saratani zinazosumbua zaidi nchini ni mlango wa kizazi, tezi dume ambayo inasababisha vifo kwa asilimia 19 na saratani ya matiti.

“Mapambano haya yanahitaji nguvu ya pamoja na ili tuweze kufanikisha vita hii tunapaswa kukinga, kutoa elimu na matibabu. Watu wafundishwe na kuelewa nini cha kufanya, wafanye kazi zinazotumia nguvu na kutoka jasho ili kudhibiti mwili kuongezeka na kuwa na uzito uliopitiliza.

“Wafanye uchunguzi wa mara kwa mara kuanzia wanapofikisha umri wa miaka 25, kupima uzito, kupima shinikizo la damu, kuangalia hali ya sukari kwenye damu, kuchunguza saratani mbalimbali,” amesema.

Naye Rais wa KGA, Dk. Lulu Sakafu, amesema kwa siku tatu watatoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Kituo cha Afya Buguruni na Hospitali ya Chanika ambapo watafanya uchunguzi wa shinikizo la juu la damu, sukari, saratani ya matiti, saratani ya mlango wa kizazi na kupima uwiano wa uzito na urefu.

“Katika jitihada za kuboresha afya za Watanzania na kujenga taifa lenye nguvu kazi ya kutosha kwa maendeleo ya nchi, mwaka huu KGA imeangalia namna ya kukabiliana na mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza kwa jamii katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kwenye changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza ukiona dalili unakuwa umechelewa ndiyo maana tumeona tuwekeze kwa kutoa elimu,” amesema Dk. Sakafu.

Dk. Sakafu amesema pia wametengeneza studio itakayotumika kurekodi vipindi vifupi ambavyo vitasambazwa katika maeneo mbalimbali ya umma ili kujenga uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa yasiyoambukiza.

Kwa mujibu wa Dk. Sakafu, tangu chama hicho kianzishwe mwaka 2017 kimekuwa kikitekeleza shughuli tofauti kama vile usimamizi wa vifaa vya kitabibu, mafunzo kwa watumiaji wa vifaa, mafunzo kuhusu usalama barabarani kwa ajali za pikipiki, huduma ya kwanza, uhamasishaji wa jamii na mafunzo ya kuokoa maisha kwa wagonjwa mahututi.

Amesema hadi sasa mikoa 12 imenufaika ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Mbeya, Iringa, Kigoma, Arusha, Mwanza, Geita, Mwanza, Shinyanga na Singida.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Ilala ambaye alikuwa mgeni rasmi, Charangwa Selemani, amesema ni muhimu kuchukua hatua madhubuti za kukinga na kutibu kabla magonjwa hayo hayajaleta madhara makubwa.

“Hivi sasa kuna janga kubwa la magonjwa yasiyoambukiza na visababishi vikubwa ni mtindo wa maisha, kama Serikali tuongeze nguvu kutoa elimu ya afya ya akili kupunguza matatizo ya ajabu yanayoendelea kutokea nchini,” amesema Selemani.

Related Posts