DC Kilombero ampa siku 16 mkandarasi kukamilisha matengenezo reli ya Tazara

Mlimba. Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya ameongoza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kukagua matengenezo ya reli ya Tazara iliyosombwa na maji katika eneo la Lumumwe, kata ya Mlimba kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo Mei 9, 2024, Kyobya amemtaka mkandarasi aliyepewa kazi ya matengenezo ya reli hiyo kuifanya usiku na mchana ili safari za Dar es Salaam kwenda Makambako ziendelee kama awali.

Kyobya  amesema “Kukwama kwa reli hii kunaathiri uchumi wa halmashauri ya Mlimba na hata wananchi kwa ujumla kwa sababu wasafiri na wafanyabiashara waliokuwa wakitoka Makambako na Mbeya kuja hapa kwa shughuli za kibiashara, kwa sasa hawafiki,” amesema Kyobya.

Hivyo, amemtaka mkandarasi huyo ambaye yuko chini ya Tazara kuhakikisha matengenezo yanakamilika ifikapo Mei 25,2024  ili safari za Dar es Salaam – Makambako zianze.

Kwa upande wake, Mkuu wa Stesheni ya Mlimba, Alex Mhini amesema kwa sasa matengenezo yanayofanywa ni kuweka karavati ili kuunganisha kipande cha reli kilichosombwa na maji.

“Wahandisi wanaofanya matengenezo haya wanasema mvua ndiyo iliyofanya kazi hiyo ichelelewe kumalizika, mwanzoni walitegemea kukamilisha kazi hiyo Mei 15 lakini kutokana na mvua zilizonyesha wiki mbili zilizopita, haijakamilika kwa wakati na sasa wanategemea kuikamilisha Mei 25 kwa kuwa hali ya hewa ni nzuri,” amesema Mhini.

Amesema safari zinazoendelea sasa ni za kutoka Mlimba hadi Dar es Salaam kwa kutumia treni ya Mwakyembe ambapo zinazofanywa  mara mbili kwa wiki.

Related Posts