Nyakati muhimu za sherehe hiyo inayotarajiwa kuanza saa moja usiku majira ya Ufaransa, itakuwa kuifungua milango mikubwa ya kanisa hilo kongwe lenye miaka karibu 900, kupigwa kengere yenye mlio unaosikia eneo kubwa la mji wa Paris pamoja na misa ya kwanza tangu kanisa hilo kuteketea kwa moto zaidi ya miaka 5 na nusu iliyopita huku chanzo cha moto huo kikiwa hadi sasa hakijafahamika.
Jumamosi jioni, waumini wa Kikatoliki wapatao 1,500 wana shauku ya kufanya tena ibada ndani ya Kanisha hilo linalofahamika kama “Notre Dame de Paris” , ibada itakayoongozwa na Askofu Mkuu Laurent Ulrich, huku misa kuu ya uzinduzi ikifanyika hapo kesho Jumapili ambapo baadaye kanisa hilo litafunguliwa kwa umma kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa mbili usiku, lakini kunatarajiwa watu wengi.
Ufaransa na Kanisa Katoliki wanaichukulia sherehe hiyo itakayopeperushwa moja kwa moja kwenye runinga kama fursa ya kuonyesha ujasiri na kudhihirisha ushawishi wao kimataifa. Rais mteule wa Marekani Donald Trump, mke wa rais wa sasa wa Marekani Jill Biden, Mwanamfalme William wa Uingereza na wakuu wa nchi na serikali wapatao 50 watahudhuria.
Ujio wa viongozi hao ni ushindi mkubwa wa kidiplomasia kwa rais Macron hasa kutokana na sherehe hizo kuhudhuriwa na Trump ambaye itakuwa safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu aliposhinda uchaguzi.
Tukio la kuungua Kanisa na mshikamano wa kimataifa
Aprili 15 mwaka 2019 tukio la kuungua kwa Kanisa hilo lilizusha hali ya mshituko na masikitiko makubwa kuona jengo hilo lenye utajiri wa kihistoria likiteketea kwa moto. Mamlaka za Ufaransa
zilisema tukio hilo halikusababishwa na uchomaji wa makusudi na kusema kuwa huenda chanzo ni hitilafu ya umeme au sigara ambayo haikuzimwa.
Kwa haraka sana michango ilianza kutolewa ili kulikarabati kanisa hilo ambapo kwa jumla, watu 340,000 kutoka nchi zaidi ya 150 walichangia dola milioni 888, msaada ambao ulidhihirisha mshikamano wa kimataifa ambao ulivuka mipaka ya kiimani.
Soma pia: Viongozi wa dunia wakusanyika Paris kwa ajili ya Notre-Dame
Usiku huo Kanisa la Notre Dame lilipoungua, Rais Emmanuel Macron aliahidi kulikarabati katika kipindi cha miaka 5. Atakapohudhuria sherehe za ufunguzi hivi leo, Macron anayekabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa baada ya serikali ya Waziri wake mkuu Michel Barnier kuangushwa na Bunge, anaweza kujivunia kwamba lengo hili limefikiwa licha ya mashaka yaliyokuwa yakitolewa na baadhi ya waangalizi.
Baada ya ukarabati huo, maafisa wa Ufaransa wamesema Kanisa hilo limekuwa zuri zaidi kuliko hapo awali, kwa sababu paa na vitu vingine vilivyoharibiwa na moto huo vilijengwa upya na maelfu ya mafundi wataalam, lakini pia kuta na michoro iliyokuwa imechakaa kwa miaka mingi imesafishwa au kubadilishwa, hasa ikizingatiwa kuwa si maeneo yote yaliyoharibiwa kwa moto.
(Vyanzo: AP, DPA, Reuters, AFP)