Ken Gold imekuwa timu ya kwanza Ligi Kuu Bara kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa penalti 4-3 na Mambali Ushirikiano kufuatia dakika 90 zilizomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mambali Ushirikiano inashiriki Ligi Daraja la Tatu Mkoa wa Tabora ambapo inaweka rekodi tamu ya kuiondoa timu ya Ligi Kuu katika hatua za awali ya michuano hiyo.
Mchezo huo ambao ulianza ulichezwa jana Ijumaa katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ulishindwa kumalizika kutokana na kujaa maji na kuendelea leo, Jumamosi.
Wakati mechi hiyo ikiahirishwa, timu zote zilikuwa hazijafungana kabla ya mwendelezo wa kumalizia dakika 90 kwa Ken Gold kupoteza ikipata kipigo hicho.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Jose Mkoko amesema pamoja na matokeo hayo ya kuumiza, lakini kwa sasa wanaelekeza nguvu kwenye mechi za Ligi Kuu.
“Hakuna namna tunaenda kujipanga upya na mwendelezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo, Simba na Singida Black Stars. Tumeumizwa na matokeo haya,” amesema Mkoko.
Timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza haijawa na matokeo mazuri ikiwa mkiani kwa pointi sita baada ya kucheza mechi 13.