KIWANGO bora kinachoonyeshwa na baadhi ya viungo wa Singida Black Stars waliochangia mabao 10 kati ya 16 ya timu nzima, yanamtesa kiungo nyota wa kikosi hicho, Najim Mussa ambaye amekuwa akisotea benchi licha ya uwezo mkubwa aliokuwa nao.
Nyota huyo aliyejiunga na Singida msimu huu akitokea Tabora United, mambo yamekuwa tofauti kwake kwani hadi sasa ameanzia benchi michezo miwili tu kati ya 12 ambayo kikosi hicho kimecheza.
Najim ameshindwa kupenya kutokana na viungo Emmanuel Keyekeh aliyetokea FC Samartex ya Ghana, Josaphat Arthur Bada aliyetoka Asec Mimosas, huku mwingine akiwa ni Mohamed Damaro aliyetoka Hafia FC ya Guinea.
Nyota hao wamechangia mabao 10 kati ya 16 yaliyofungwa msimu huu na Keyekeh amefunga mawili na kuchangia pia mawili’, huku Josaphat akitupia mawili na kuasisti matatu, wakati Damaro amefunga moja.
Akizungumzia hali hiyo, Najim alisema licha ya kutopata muda mwingi wa kucheza ataendelea kupambana kadri atakavyopewa nafasi, huku akidai changamoto iliyopo anaichukulia ni fursa ya kumkuza kiakili.
“Naamini ushindani huu uliopo pia unanifanya kuongeza juhudi zaidi uwanjani. Nawaheshimu waliopo na nitaendelea kupambana kila nitakapopewa nafasi,” alisema Najim.