SERIKALI inakusudia kumuweka kikaangoni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mohammed Enterprises Limited (MeTL), Mohammed Dewji, kumhoji iwapo ameshindwa kuendesha kiwanda na mashamba ya chai, yaliyoko wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga, ili yachukuliwe kwa ajili ya kumpatia mwekezaji mwingine.
Pia anadaiwa kushindwa kuyaendeleza mashamba na mitambo ya viwanda vya chai huko Rungwe mkoani hali inayosababisha wakulima kukosa masoko. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, baada ya Mbunge wa Korogwe, Timotheo Mzava (CCM), kuwasilisha hoja ya dharura akiutaka mhimili huo kujadili changamoto ya kukosa masoko inayowakabili wakulima wa chai baada ya viwanda viwili vilivyoko wilayani Korogwe ikiwemo cha Mo Dewji, kufungwa kwa muda wa miezi miwili.
Bashe amedai kuwa, wizara yake ilituma timu ya wataalamu kufanya tathmini juu ya mashamba ya chai aliyokabidhiwa Mo Dewji ili kubaini kama aliyafanyia uendelezaji na kama ana nia ya kuendelea kufanya uwekezaji.
Pia, amesema walimwandikia barua Mo Dewji ya kumtaka kutofunga kiwanda kwa sababu kuna wakulima wadogo wanaotegemea kuuza chai yao kiwandani hapo, lakini aliamua kufunga.
“Ile ni mali yake lakini ilikuwa mali ya umma aliyouziwa kwa makubaliano maalum na Serikali, kama wizara tunaomba mtupe nafasi sasa hivi timu yetu ya wizara itamuita kama ana nia ya kuendeleza mashamba haya tutayachukua kama serikali, tutayafanyia tathmini kutokana na hali iliyokuwepo sasa,” amesema Bashe.
Bashe amesema, wizara yake imepata idhini kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuyachukua mashamba hayo itakapobainika kama Mo Dewji hana nia ya kuyaendeleza kama inavyotakiwa na kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwepo.
Amesema, kabla ya vikao vya Bunge la Bajeti linalotarajiwa kuisha Juni mwaka huu havijafika tamati, wizara yake itawasilisha taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa kuhusu suala hilo, huku akihakikisha kwamba Serikali inachukua hatua za ziada kunusuru soko la zao la chai.
Baada ya maelezo hayo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka Wizara ya Kilimo ihakikishe viwanda hivyo vinafunguliwa ili chai ya wakulima iliyoko tayari kuvunwa ipate soko na kuwaepusha wakulima na hasara.