Dar es Salaam. Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa (Sura ya 290) ya mwaka 1982, inatoa mamlaka kwa halmashauri za wilaya, manispaa au miji kutunga sheria ndogo kuhusu matumizi ya maeneo ya biashara.
Pia inatoa mamlaka kwa halmashauri kudhibiti na kupanga shughuli za kibiashara katika maeneo yao.
Licha ya kuwapo maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya biashara, bado wafanyabiashara maarufu Machinga wanapanga bidhaa barabarani jijini Dar es Salaam.
Ufanyaji huu holela wa biashara unakiuka sheria na kanuni mbalimbali zinazohusu utaratibu wa matumizi ya ardhi, usalama wa raia na usafi wa mazingira.
Kwa mfano, Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 inakataza matumizi ya barabara kwa shughuli zisizokusudiwa, kama vile biashara, ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wake.
Biashara barabarani huchangia msongamano na ajali, kinyume cha sheria inayotaka udhibiti wa matumizi sahihi ya barabara.
Si hivyo pekee, Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 inaeleza ardhi ya barabara na maeneo ya umma hayaruhusiwi kutumiwa kwa biashara binafsi bila idhini rasmi.
Ufanyaji biashara barabarani huchangia uchafuzi wa mazingira kwa kutupa taka ovyo, hivyo kwenda kinyume cha Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Wafanyabiashara wanaopanga bidhaa barabarani mara nyingi wanazuia njia, jambo linalokiuka sheria za usalama wa umma, hivyo kuathiri huduma za dharura kama vile magari ya zimamoto au ya wagonjwa.
Kutokana na ukiukaji wa sheria na kanuni zilizopo, kumekuwa na msongamano wa magari na watu, hivyo kusababisha ucheleweshaji wa shughuli.
Katika maeneo kama vile Kariakoo, Mbezi, Mbagala na Tandika, barabara nyingi zimejaa meza kwa ajili ya biashara, bidhaa nyingine zimetandazwa chini, kuna mikokoteni na wafanyabiashara baadhi wakitumia vipaza sauti kunadi bidhaa zao.
Kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (1) hifadhi ya barabara ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na upanuzi wa barabara au shughuli nyingine zinazohusiana na barabara pekee.
Akizungumza na Mwananchi Mwenyekiti wa Wamachinga, Namoto Yusuph amesema yanayoendelea sasa ni usimamizi hafifu wa makubaliano baina yao na mamlaka husika.
Amesema walikubaliana na Serikali na walipewa mitaa tisa katika eneo la Kariakoo ambayo ni Congo, Nyamwezi, Swahili, Sikukuu, Aggrey, Mchikichi, Muhonda, Narung’ombe na Tandamti kwa ajili ya kupanga meza za chuma kushoto na kulia katikati wakiacha njia.
“Katika makubaliano yetu mitaa ya Msimbazi na Uhuru, itasimamiwa na askari wa jiji ili kuhakikisha wamachinga hawavunji sheria na makubaliano tulioweka ya kufanya biashara katika mitaa hiyo lakini imekuwa tofauti,” amesema.
Kutosimamiwa kwa jambo hilo anasema wamachinga wamerudi kwa kuongezeka kila siku kwani awali walikuwa 5,000 lakini kwa sasa wapo zaidi ya 15,000 na wanaendelea kuongezeka kutoka shuleni na vyuoni.
Kutokana na ukosefu wa ajira, baada ya masomo wahitimu wamekuwa wakijiingiza kwenye biashara ili kuendesha maisha yao.
“Hakuna chombo kinachoweza kusema eneo fulani limejaa, hivyo angalieni maeneo mengine kwa kuwa hakuna mfumo wa kanzi data, hivyo wanashindwa kuwasimamia waliopo,” amesema.
Tofauti na hilo amesema usimamizi wa maeneo ambayo wamewaondoa wamachinga ni tatizo kwa kuwa yanatumiwa na wenye maduka kuweka bidhaa zao na kuegeshwa pikipiki na bajaji.
Namoto ameshauri mamlaka husika kuitisha mdahalo ukihusisha wadau ili kupata maoni ya nini kifanyike na kutoa suluhisho la kudumu kuliko kutoa matamko.
“Kwa sababu hakuna ushirikishwaji katika mipango, matokeo yake wanatoa matamko ambayo anayeambiwa hajui. Suluhisho ni kuita wadau ili kupata maoni ya nini kinaweza kufanyika kuondoa kero, ikiwemo ya nafasi ya vizimba kwenye masoko yenye wateja,” amesema.
Desemba 5, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwa katika uzinduzi wa mikopo ya asilimia 10 na vitambulisho vya ujasiriamali, alisema wafanyabiashara kukaa kila mahali si sawa.
“Hii biashara ya kukaa kila mahali wafanyabiashara wenzangu hapana, juzi lile ghorofa mmeliona limedondoka pale Kariakoo namna ya kupeleka fire (gari la zimamoto) na mitambo imetulazimu tufunge mitaa karibu wiki nzima,” alisema.
Novemba 16, jengo la ghorofa katika mtaa wa Congo na Mchikichi liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 31 na wengine 88 kuokolewa.
Chalamila alisema kila mahali mtaa haukuwa ukiingilika, haupitiki, hivyo muda si mrefu wataelekezana kupanga tena upya biashara.
“Halafu pia biashara hizi hatuwezi tukawa tunapanga vitu pale kuna mafremu yamejengwa Ubungo na Wachina kwa kushirikiana na Serikali mkakodi mmeshakua, mnapokua mumshukuru Mungu,” alisema.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wanasema kuondolewa bila kupatiwa maeneo rasmi, kunawaweka katika hali ngumu ya maisha.
“Hii ni biashara yetu pekee tunayoitegemea, tukiambiwa tuondoke bila kuonyeshwa wapi pa kwenda, tunashindwa hata kuendesha familia,” amesema Ahmed Juma, mfanyabiashara wa viatu mtaa wa Narung’ombe, Kariakoo.
“Wateja wanapenda kununua hapa kwa sababu ni rahisi kufika. Masoko rasmi yako mbali na gharama za kulipia ni kubwa,” amesema Neema Hamis, mfanyabiashara wa nguo za watoto katika mtaa huo.
Anthony Mwita, amesema gharama za kupanga eneo la biashara ni kubwa, ndiyo sababu ya wao kupanga bidhaa barabarani.
“Nauza chaja za simu na makasha yake ni ngumu kuwaza kupanga fremu ndiyo maana nakimbizana na mgambo, maana napata kipato kidogo na wakati huohuo ninapoishi pia natakiwa kulipa kodi,” amesema Mwita.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema vijana wanaendelea kufanyabiashra barabarani kwa sababu hakuna nafasi ya ajira.
“Wanaofanya kazi ya umachinga wengi wao ni vijana ambao wamemaliza sekondari na vyuo vikuu, na hata wengine hawajabahatika kusoma kwa namna moja au nyingine na kila siku wanaendelea kuongezeka,” amesema.
Amesema kila mwaka shule na vyuo vinatoa wahitimu, kwa hiyo Serikali ikipanga maeneo leo wanaweza kukaa sawa lakini baada ya miaka miwili wakarudi tena barabarani kwa sababu wameongezeka.
Ili kupunguza adha hiyo, amesema Serikali iwekeze kwenye kilimo kwa ajili ya uzalishaji, huku kukifunguliwa viwanda vingi vya uzalishaji na uchakataji ambavyo vitaajiri watu wengi.
“Viwanda ni sehemu pekee ambayo inaweza kuajiri watu wengi na ikifanikiwa kufanya hivi hakuna kijana atakayekubali kwenda barabarani ambako hana uhakika wa kuhudumia afya yake na kupata kipato cha siku,” amesema.
Amesema watu wengi wanataka maisha ya uhakika ikiwepo huduma ya afya, kupata mshahara utakaosaidia mahitaji yake, hivyo ni ngumu kulazimisha kurudi barabarani ambapo hana kipato cha uhakika.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Jane Prosper amesema suala la wamachinga ni changamoto ya kiuchumi na kijamii inayohitaji suluhisho la kudumu, ili kufanikisha maendeleo endelevu kwa pande zote.
“Wafanyabiashara hawa wanachangia uchumi wa kila siku wa jiji kwa kuwezesha mzunguko wa fedha kupitia biashara zao ndogondogo, ambazo mara nyingi hutegemewa na wananchi wa kipato cha chini,” amesema.
Amesema changamoto hiyo inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na wafanyabiashara wenyewe.
“Serikali inapaswa kuunda mpango madhubuti wa kuwapatia maeneo rafiki na rasmi kwa biashara zao, hili litasaidia siyo tu kurahisisha shughuli za kijamii, bali pia kuongeza mapato ya Serikali kupitia ushuru wa masoko na kupunguza gharama za usimamizi wa miji.
“Ni muhimu pia kuzingatia ustawi wa wamachinga kwa kuhakikisha hawapotezi wateja wao au kipato chao wakati wa mpito huu,” amesema.
Amesema ni vyema suluhisho lolote liwe la muda mrefu na lenye uwiano wa kijamii, kiuchumi, na kisheria.
“Suluhisho la kudumu litakuwa na athari chanya kwa uchumi wa jiji na ustawi wa wananchi wote, huku likihakikisha maendeleo ya miundombinu yanaendana na mahitaji ya wakazi wa mijini,” amesema.