Serikali yaahidi ushirikiano na sekta binafsi, kutatua changamoto

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha ustawi na maendeleo ya biashara nchini.

Wataalam kutoka taasisi mbalimbali walioshiriki mjadala katika Kongamano la biashara na uwekezaji baina ya serikali na sekta binafsi akiwemo Mkurugenzi wa Usalama na Afya wa OSHA, Dk. Jerome Mteru (wa pili kushoto).

Ametoa kauli hiyo ya serikali wakati akifungua kongamano la mwaka la majadiliano ya biashara na uwekezaji kati ya serikali na sekta binafsi lililoandaliwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na kufanyika jijini Dar es Salaam Desemba 6 hadi 7, 2024.

“Kwa niaba ya serikali nichukue fursa hii kuishukuru sana sekta binafsi kwani mmendelea kuiunga mkono na kuwa na imani na Serikali ya Awamu ya Sita naleo tunashuhudia maendelea makubwa na ya haraka ya kibiashara na uwekezaji hapa nchini,” ameeleza Naibu Waziri Mkuu na kuongeza:

“Niwahakikishie kwamba serikali itaendelea kushirikiana nanyi sekta binafsi ili kuwezesha na kutekeleza yale yote mnayoyaona kuwa ni changamoto kwenye biashara zenu ili tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu kwa pamoja,”

Amebainisha mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi kupitia kodi na kutoa ajira kwa idadi kubwa ya watu.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi, (OSHA), Khadija Mwenda akitia saini ya hati ya makubaliano ya mashirikiano (MoU) kati ya OSHA na TCCIA, katika kongamano la majadilino ya biashara na uwekezaji kati ya serikali na sekta binafsi mwaka 2024, lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa Barani Afrika na Tanzania ikiwemo inakisiwa kwamba vijana takribani milioni 12 wanaingia katika soko la ajira kila mwaka ambapo asilimia 25 tu hupata ajira serikalini na asilimia 75 huajiriwa na sekta binafsi.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu, miaka ya hivi karibuni kulikuwa na malalamiko toka kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu uwepo wa sheria na taratibu za kiserikali zinazokwamisha maendeleo ya biashara ambapo ameeleza kuwa serikali ilifanyia kazi malalamiko tajwa jambo lililopelekea kufutwa kwa tozo zaidi ya 374 ikiwa ni pamoja na kuondoa mwingiliano wa majukumu baina ya Taasisi za Serikali na kupunguza muda uliokuwa ukitumika kupata huduma mbalimbali za serikali kutoka siku 14 hadi siku tatu pekee.

Akitolea mfano wa tozo zilizoondolewa na serikali, Naibu Waziri Mkuu amezungumzia tozo zilizoondolewa kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) zenye thamani ya zaidi ya bilioni 35 kila mwaka, amesema kutokana nia njema ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, serikali imeamua kuziacha fedha hizo mikononi mwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akihutubia katika kongamano la majadiliano ya biashara na uwekezaji kati ya serikali na sekta binafsi lililofanyika jijini Dar es Salaam, Desemba6, 2024.

Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akitoa ufafanuzi kuhusu hati ya makubaliano ya mashirikiano baina ya OSHA na TCCIA ambayo ilisainiwa katika mkutano huo, alieleza kuwa Taasisi ya OSHA ipo kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kuweza kufanikisha malengo yao na kutoa mchango wao katika kukuza Uchumi wa nchi.

“Pamoja na jitihada za serikali yetu kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuondoa tozo zaidi ya 16 zilizokuwa zikitozwa na OSHA bado tunayo nia ya kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji nchini kupitia kuwa na mashirikiano katika nyanja mbalimbali,”ameeleza Mwenda.

OSHA ni miongoni mwa Taasisi mbalimbali zilizosaini hati za mashirikiano na TCCIA katika mkutano huo ambapo makubaliano hayo yanalenga kushirikiana katika kutoa elimu na kuhamasisha uzingatiaji masuala ya usalama na afya kwa wanachama wa TCCIA, kubadilishana taarifa mbalimbali na kufanya tafiti pamoja.

Related Posts