Polisi waja na mapya kushambuliwa  kwa maofisa TRA

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam limesema halitawavumilia watu wanaotaka kujenga tabia ya kuwashambulia watumishi wa Serikali wakati wanapotekeleza majukumu yao kisheria.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema licha ya watumishi wa Serikali kufuata taratibu za kiutendaji, bado kuna tabia inataka kujengeka “ya watu kutaka kuwashambulia kwa sababu mbalimbali zisizokubalika.”

 “Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, halitasita kuchukua hatua kali za kisheria na za haraka dhidi ya wahusika, ikiwemo kuwahoji, kuwakamata na kuwafikisha kwenye mamlaka zingine za kutenda haki,” amesema Muliro.

Muliro ameeleza hayo leo Jumamosi Desemba 7, 2024 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu tukio la kushambuliwa maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambalo lilisababisha dereva wa taasisi hiyo, Iman Simbayao kufariki dunia.

Tukio hilo lililotokea Desemba 5, 2024 saa tatu usiku eneo la Tegeta kwa Ndevu, wilayani Kinondoni ambapo maofisa wa TRA walizuia gari aina ya BMW x6 lililodaiwa kutokuwa ndani ya mfumo wa mamlaka hiyo.

Watumishi wa TRA hao walipojaribu kulizuia, gari hilo kuliibuka mzozo hadi dereva akapiga kelele kuomba msaada akidai anatekwa, jambo lililosababisha wananchi kuwashambulia kwa mawe maofisa wa TRA.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka matukio ya watu kukamatwa yanayohusishwa na utekaji, huku mengine yakihusisha watendaji wa vyombo vya dola.

Katika maelezo yake Muliro amesema ni lazima jamii kujenga tabia za kuheshimu mamlaka zilizowekwa kisheria wakati wa kutimiza majukumu ya kisheria.

“Hatuwezi kwenda na mtazamano huo ni sawasawa na mtu anayefanya wizi, halafu unasema kwa sababu kuna njaa sasa afanye nini wakati hakuna chakula. Kuna kikiundi cha watu wachache kinafanya makosa, basi kila mtu hataki kukamatwa pindi anapotenda kosa kwa mwamvuli wa kuonekana anataka kutekwa.

“Kwa hiyo twende na huo utaratibu, yaani wezi wajifanyie wanavyoweza, wakitaka kukamatwa waseme tutaamini vipi ni polisi? Tutaendelea kuwashughulikia wahuni hawa,” amesisitiza Muliro.

Katika mkutano huo, Muliro amesema Jeshi la Polisi linawashikilia Deogratius Masawe na Bakari Idd (wabeba mizigo), Omary Issa (mpiga debe) na Rashid Mtonga (mwendesha bodaboda), kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Simbayao.

“Hawa watu wanne waliokamatwa na wengine wanaohojiwa kwa kina, wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya mtumishi wa TRA, Aman Simbayao na kumjeruhi mwingine Adriano Fredrick,”

“Watuhumiwa hawa wakati wakiwashambulia maofisa hao waliahiribu pia gari la TRA. Tukio hili lilitokea baada ya maofisa hawa TRA kukamata gari ambalo lilidaiwa kuwa na makosa ya kikodi,” amesema Muliro.

Muliro amesema watumishi hao wa TRA walikuwa wakiteleza jukumu hilo kisheria kwa kufuata taratibu zote dhidi ya mtuhumiwa, lakini lilijitokeza kundi la watu, wakiwemo watuhumiwa wanne walioshambuliwa kwa mawe na baadaye kusababisha kifo cha Simbayao.

Related Posts