Waitwa kuchangia ufadhili wa masomo fani ya urubani

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kufanyia maboresho usafiri wa anga kwa kuongeza ndege na kutengeneza miundombinu wezeshi, wito umetolewa kwa wadau wa sekta hiyo kuchangia mfuko utakaowezesha kusomesha vijana wa Kitanzania ili kuondoa utegemezi wa wageni.

Inaelezwa kuwa kwa sasa kuna Watanzania wachache wanaohudumu kwenye fani za urubani na uhandisi wa ndege, hali inayotoa mwanya kwa wenye fedha na watu wa mataifa ya nje, kuchangamkia fursa hizo huku vijana kutoka familia maskini wakiendelea kuwa watazamaji.

Kufuatia hilo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Ramadhan Msangi amewataka wadau wa sekta hiyo kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko kwa kushiriki kuwasomesha Watanzania wenye utayari na sifa za kusoma kozi hizo.

Ombi hilo la Msangi amelitoa leo Desemba 7, 2024 ambapo Tanzania kupitia TCAA imeungana na mataifa mengine kuadhimisha miaka 80 ya usafiri wa anga.

Amesema uwekezaji mkubwa unaofanyika katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kutanua wigo wa biashara ya usafiri wa anga kwa kuingia ushirikiano na mashirika mbalimbali, unapaswa kwenda sambamba na kuongeza wataalamu.

“Mwaka 2016 tulikuwa na ndege moja lakini sasa tuna ndege 16, mashirika makubwa yanaleta ndege zao nchini na tumekuwa tukiingia makubaliano ya ushirikiano na mataifa mengi, hii yote inakuza na kuchangamsha sekta ya usafiri wa anga.

“Jitihada hizi zinapaswa kwenda sambamba na uwepo rasilimali watu wa kutosha kwenye sekta. Kutokana na gharama kubwa za mafunzo ya fani za urubani na uhandisi wa ndege, Watanzania wengi wanashindwa kusoma kozi hizo hivyo inakuwa fursa kwa wageni. Mwanafunzi mmoja gharama yake inafika Sh200 milioni,”amesema

Msangi amesema kukabiliana na changamoto hiyo ya upungufu wa marubani na wahandisi wa ndege wazawa, TCAA ilianzisha mfumo wa kuwasomesha vijana wa Kitanzania ambao katika awamu ya kwanza imetoa wahitimu wanane.

“Kupitia michango ya wadau tulifanikiwa kupeleka masomoni kundi la kwanza la vijana waliokwenda kujifunza urubani, hatimaye wamemaliza na wako tayari kuingia kwenye soko wakiwa na vigezo vyote vya kurusha ndege.

“Nitumie fursa hii kuwaomba wadau wa sekta ya usafiri wa anga kuendelea kuchangia mfuko ili tuweze kugharamia mafunzo ya marubani wetu wazawa, pia wawapokee hawa wanaohitimu kwa sababu wameshaiva na wako tayari kufanya kazi ndani na nje ya nchi,” amesema Msangi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake waliohitimu mafunzo ya urubani,  Wardat Hamid ametoa shukrani zake kwa mamlaka na wadau waliofadhili mafunzo yao, kwa kile alichoeleza isingekuwa ufadhili huo ni ngumu kwa vijana kutoka familia za kawaida kumudu gharama.

“Inawezekana vijana wengi wana ndoto ya kuwa marubani lakini wanashindwa kusoma kutokana na gharama kubwa. Sisi tumewezeshwa hatuna budi kushukuru kwa fursa hii na niombe isiishie kwetu kwani wahitaji ni wengi.

“Nitumie fursa hii kuwasihi watoto wa kike kuchangamkia masomo ya sayansi kwa kuwa ndiyo njia ya kufikia ndoto mbalimbali ikiwemo hii ya urubani. Wito wangu kwa wadau mtupokee kwenye soko kwa kuwa tuko tayari kuwahudumia,” amesema Wardat.

Related Posts