Dar es Salaam. Siku tatu zijazo nchi za Kenya na Tanzania zitaweza kufanya biashara ya umeme baada ya kuwashwa kwa njia ya msongo wa kilovoti 400 inayounganisha mataifa hayo mawili vinara kiuchumi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Hatua inayotarajiwa kuongeza juhudi za kupunguza mgao wa umeme na kukabiliana na hitilafu za umeme baina ya nchi hizo mbili huku ikiifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu baada ya Ethiopia na Uganda kufanya biashara ya umeme na Kenya.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba aliliambia Mwananchi kuwa kwa hatua hiyo mtandao wa umeme wa Kenya na Tanzania utakuwa umeunganishwa na kila nchi itakuwa na uwezo kuisambazia umeme nchi nyingine pindi kunapokuwa na upungufu.
“Kuwashwa kwa njia hiyo maana yake tunaweza kusambaziana umeme, yaani tunaweza kuuza huko na wao wanaweza kuuza kwetu. Uzuri sisi tuna umeme wa ziada hivyo tunaweza kuwauzia wakiwa na uhitaji,” amesema Mramba.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usambazaji Umeme la Kenya (Ketraco), Dk John Mativo, juzi aliiambia gazeti la Business Daily la nchini Kenya kuwa kwamba njia ya kusafirisha umeme inayounganisha nchi hizo mbili itaanza kufanya kazi rasmi Desemba 11, 2024.
Miezi kadhaa iliyopita, mashirika ya umeme ya nchi hizo mbili yamekuwa yakifanya majaribio ya laini hiyo ya umeme yenye thamani ya Dola 309.26 milioni (Sh804.3 bilioni), kujiandaa kwa hatua ya kuiwasha rasmi.
Pande zote mbili zinaitazama hatua hii ya uwashaji wa njia hii ya umeme kama ya kuleta mageuzi makubwa kwa nchi zote mbili, kwani utawezesha kuuza umeme wa ziada na kununua kutoka nchi jirani iwapo kutakuwa na upungufu wa uzalishaji.
Lakini hii itakuwa na faida kubwa kwa Kenya, ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya uzalishaji wa kutosha wa umeme wa kukidhi mahitaji yake na changamoto ya mgao inayokabili taifa hilo la kwanza kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Uanzishaji wa laini hii unakuja miezi miwili baada ya Kenya Power kusaini mkataba wa kubadilishana umeme na Shirika la umeme Tanzania (Tanesco), ambayo ni msambazaji pekee wa umeme nchini Tanzania.
“Vituo vya Kitaifa vya Kudhibiti Umeme vya Kenya na Tanzania vimeruhusu Ketraco, Kenya Power, na Tanesco kuwasha laini hiyo Jumatano, Desemba 11, 2024. Tunaomba mambo yaende kama ilivyopangwa,” alisema Dk Mativo.
Zaidi ya hayo, njia ya umeme kati ya Kenya na Tanzania itaunganishwa na mfumo wa usafirishaji umeme wa Ethiopia-Kenya kupitia laini ya Isinya-Suswa yenye uwezo wa kilovoti 400. Laini hii ni sehemu ya Mradi wa njia ya umeme ya Afrika Mashariki inayoweza kusafirisha megawati 2,000.
Laini hii ya Kenya-Tanzania ni kiungo muhimu sio tu kati ya nchi hizo mbili, kadhalika inaunganisha Ethiopia na Tanzania. Ethiopia tayari inapanga kuuza megawati 100 za umeme kwa Tanzania kupitia Kenya.
Hivi karibuni Tanzania imeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa uzalishaji wa umeme wa ndani kwa kujenga Mradi wa Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) lenye uwezo wa megawati 2,115.
Novemba 05, Mwaka huu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko alieleza kuwa uzalishaji wa umeme uliounganishwa katika gridi ya Taifa ulifikia Mega wati 2,607 huku megawati 1,175 zikitoka katika mradi wa JNHPP.
Aidha laini ya umeme ya Kenya-Tanzania pia ni nguzo muhimu ya Jumuiya ya Umeme ya Afrika Mashariki (EAPP), ambayo inajumuisha kundi la nchi 13 kutoka kanda hiyo zinazotaka kufanya biashara ya pamoja ya kuuziana umeme.
Kenya ilianza kuagiza umeme kutoka Ethiopia Desemba 2022 kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa ununuzi wa umeme kati ya mashirika yao mawili ya umeme Julai mwaka huo. Hata hivyo, shughuli kamili za kibiashara za mkataba huo zilianza Desemba 2023.
Kenya pia inaagiza umeme kutoka Uganda. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa uagizaji wa umeme kutoka Uganda na Ethiopia uliongezeka kwa asilimia 76.7 katika kipindi cha miezi tisa hadi Septemba, Kenya ikiharakisha kuepuka mgao wa umeme na kupunguza hitilafu za umeme.
Kenya iliagiza rekodi ya kilowati-saa milioni 1,137.84 za umeme kutoka Uganda na Tanzania katika kipindi hicho cha miezi tisa. Hii ilikuwa ongezeko kubwa kutoka kilowati-saa milioni 643.91 zilizoagizwa mwaka uliopita katika kipindi kama hicho, kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Kitaifa ya Kenya.
Hatua hiyo ilisaidia Kenya kuepuka mgao mkubwa wa umeme kutokana na upungufu wa uzalishaji wa ndani, ambao ulipungua kwa asilimia 0.6 hadi kilowati-saa milioni 9,339.5 katika kipindi hicho, ikilinganishwa na kilowati-saa milioni 9,399.54 mwaka uliopita.