Watimua mbio, baada ya kufutiwa kesi na DPP

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia kesi na kuwaachia huru watu 10 wakiwemo wafanyakazi wa benki ya NBC na Habib African, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuchepusha fedha na kuisababisha hasara Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania (TGFA) kiasi cha Sh2.16bilioni.

Washtakiwa hao wamefutiwa kesi hiyo na kuachiwa huru, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Waliofutiwa kesi ni Clement Kiondo (42) ambaye ni mhasibu wa benki ya Habib Africa, Devotha Masmini (52) na  Catherine Mkelo (54) ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo.

Wengine ni wafanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambao ni Samwel Kyondo (52), Fatuma Abdulaziz (52), Varelia Mhina (58) na Christopher Mduma(59).

Katika shauri hilo washtakiwa wengine ni Killian Kilindimo, mfanyabiashara Peter Tema (39) na Henry Kishaluli, ambaye ni wakili wa kujitegemea.

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 26/2023, yenye jumla ya mashtaka 48 yakiwemo ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za hundi na fedha mbalimbali, wakionyesha Ofisi ya Waziri Mkuu imeridhia fedha hizo zitolewe na kupewa kampuni ya Kalembo General Enterprise na Karimu G. Husein, kinyume cha sheria.

Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo, umetolewa jana na Desemba 6, 2024, na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada ya wakili wa Serikali Tumaini Mafuru, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

Wakili Mafuru amedai kuwa kesi hiyo ililetwa mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kusomea maelezo ya mashahidi, idadi ya mashahidi pamoja na vielelezo, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika.

“Hata hivyo, mheshimiwa hakimu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), hana nia ya kuendelea na shauri hili, hivyo anaomba mahakama yako tukufu iliondoe shauri hili mpaka hapo atakapoona inafaa kwa wakati mwingine. Hivyo tunaomba kuwasilisha maombi haya, chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022,” amedai Mafuru.

Mafuru baada ya kueleza hayo, Hakimu Lyamuya amesema kutokana na hati hiyo iliyowasilisha chini ya kifungu hicho, Mahakama inawaachia huru washitakiwa hao, kwa sababu upande wa mashtaka hauna nia ya kuendelea na kesi dhidi washtakiwa.

Hakimu Lyamuya aliwaambia washtakiwa hao kuwa kufuatia kifungu hicho kilichotumika kuwaachia huru, hakimzuii DPP kuwakamata tena na kuwafungulia mashtaka.

Wakati Hakimu Lyamuya akichambua kifungu hicho  na kukubaliana na ombi la upande wa mashtaka la kuwaachia huru, washtakiwa hao ambao kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa chemba namba 20,  walianza kusogea karibu na mlango wa kutokea na hakimu alivyotanga kuwaachia huru, washtakiwa waliparamia mlango na kutoka ndani ya chumba hicho cha mahakama huku wakikimbia, wakihofia kukamatwa tena.

Baadhi ya washtakiwa hao walisikika wakisema kwa sauti‘ askari hao watatukamata jamani kimbieni’ walisikika washtakiwa hao ambao walitoka wanakimbia hadi nje ya lango la Mahakama ya Kisutu na kisha kuvuka barabara.

Wakati washtakiwa hao wakikimbia mahakamani, mawakili wao waliwataka wasikimbie kwa kuwa hawawezi kukamatwa tena, lakini washtakiwa hao waliendelea kukimbia hadi nje ya geti na kutokomea.

Kati ya mashtaka hayo 48 mashtaka 22 ni ya kughushi 18 ya kuwasilisha nyaraka za uongo; sita ya kuchepusha fedha na mashtaka mawili ni kuongoza genge la uhalifu na kuisababishia hasara Wakala wa Ndege wa Serikali Tanzania.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, Wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Oktoba Mosi 2011 na Machi 11, 2014 katika Mkoa  wa Dar es Salaam.

Imedaiwa katika kipindi hicho washtakiwa kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu  ili kujipatia Sh2.16bilioni  kwa njia ya ulaghai, mali ya Wakala wa Wakala wa Ndege wa Serikali ya Tanzania.

Katika shtaka la kughushi na kuwasilisha nyaraka ya uongo, linalomkabili Clement na Kyondo wanadaiwa Juni 26, 2012 wilaya ya Ilala, kwa nia ya kudanganya,  walitengeneza nyaraka ya uongo ya malipo yenye thamani ya Sh542milioni wakionyesha kuwa fedha hizo zimetolewa na Wakala wa Ndege na kisha kuwasilisha nyaraka hiyo ofisi ya Waziri Mkuu, eneo la Magogoni jijini, wakati wakijua ni uongo.

Pia, Clement na Kyondo, Abdulazizi na Masmini, wanadaiwa Agosti 29, 2014, katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Viwandani, wakishtakiwa kwa pamoja walighushi nyaraka ya fedha yenye thamani ya Sh98 milioni ikionyesha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, imeridhia fedha hizo ipewe Kampuni ya Kalembo Gereral Enterprises, wakati wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Related Posts