Kiama chaja kwa madereva wa Serikali

Mbeya. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mbeya, limetakiwa kuwafungia leseni madereva wa magari ya Serikali wanaokiuka sheria za usalama barabarani.

Pia, limekumbushwa kuimarisha doria maeneo yote ya mkoa huo na kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wa barabara kuhakikisha wanazuia ajali zisizo za lazima.

Akizungumza leo Desemba 7, 2024 wakati wa kilele cha wiki ya nenda kwa usalama barabarani, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Jeshi la Polisi lisisite kuwafungia leseni madereva wa magari ya Serikali wanaokiuka sheria za barabarani.

Amewataka pia abiria kutokuwa chanzo cha ajali kwa kutokubali kupanda magari au vyombo vya moto vilivyozidi idadi kuhakikisha Mbeya inaendelea kuwa salama.

“Hao nao ni binadamu, inapotokea kuchepuka, wawe makini kwa kuwa wakipata ajali, familia zao zinaathirika lakini hata sisi viongozi tunaathirika, hivyo Polisi imarisheni doria na kuchukua hatua kwa wanaokiuka sheria.

“Niwaombe pia kabla ya kumpiga faini dereva kwa kukiuka sheria, toeni elimu kwanza ikijirudia ndio hatua zaidi zichukuliwe, lakini abiria hakikisha kabla ya kupanda gari au bajaji hakikisha kuna nafasi,” amesema Mahundi.

Mhandisi huyo ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa kuweka ajenda ya usalama barabarani kuwa kipaumbele kikubwa katika vikao vyao, akieleza kuwa Serikali inapambana kukamilisha miundombinu ya barabara nne mkoani Mbeya.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema wanaenda kutekeleza maelekezo, akieleza kuwa magari ambayo hayajakaguliwa wanataka madereva na wamiliki kuyapeleka kwa kazi hiyo.

“Tutaanza kukagua kwa lazima magari ambayo hayajakaguliwa jiorodhesheni haraka na shughuli hii tunaianza leo kuhakikisha ajali zinadhibitiwa,” amesema kamanda huyo.

Naye Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, Notker Kilewa amesema katika wiki ya nenda kwa usalama barabarani, wametoa elimu ambayo matarajio yao ni kukomesha ajali.

“Tutaendelea kutoa elimu, tumejitahidi kutumia wiki hii kufikia maeneo yote korofi ya Mkoa kwa kuongea na madereva, abiria  na wadau wa barabara kuzingatia sheria” amesema SP Kilewa.

Katibu wa madereva wa magari mkoani humo, Daniel Jackson amesema kutokana na elimu iliyotolewa pamoja na mafunzo, wanaamini ajali huenda zikapungua kama siyo kuisha.

“Tuliombe Jeshi la Polisi wanapokuja hawa madereva waliohitimu mafunzo hapa Veta Mbeya muwape leseni kwa kuwa ndio maisha yao, sisi tutajitahidi kutekeleza kwa vitendo elimu iliyotolewa,” amesema Jackson.

Mmoja wa wananchi, Jesca Mwashilindi amesema abiria na watembea kwa miguu nao ni sababu ya ajali kwa kutumia uharaka barabarani kulazimisha au kushawishi madereva kuwa na mwendo kasi.

“Muda mwingine sisi abiria tunahusika kwenye ajali, tunataka uharaka wa safari lakini hata watembea kwa miguu hawazingatii sheria wanavuka maeneo ya vivuko bila tahadhari,” amesema Jesca.

Related Posts