SERIKALI imedhamiria kujenga misingi shindani na endelevu yenye ubora wa utoaji wa huduma wenye kuwezesha biashara nchini kwa kuzingatia jiografia na rasilimali watu kwa kupitia sera mikakati na mipango shindani na shirikishi.
Ameyasema hayo jana Desemba 6, 2024 Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdalah wakati wa hafla fupi ya kupokea Cheti cha umahiri wa kutoa huduma ya Ithibati Ubora na bidhaa kutoka SADCAS iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana Jijini Dar es Salaam.
Aidha amesema cheti hicho kwa TBS ni kuthibitisha na kutafsiri maono na miongozo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan juu ya kuingia kwenye masoko ya kimataifa kwa kuwa na bidhaa bora kwani huo ni uthibitisho kuwa bidhaa inayothibitishwa na TBS inaweza kuuzwa kwenye masoko ya Kimataifa hivyo ni fursa kwa Wafanyabiashara na Wazalishaji kutumia Shirika hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Ithibati za Jumuiya ya maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADCAS) Bi. Eve Christine Gadzikwa amesema kabla ya Cheti hicho cha Umahiri katika Ithibati Ubora,TBS walishapatiwa cheti cha Umahiri katika huduma za Maabara pamoja na cheti katika mifumo ya usimamizi hivyo Shirika hilo linapiga hatua kubwa kwenye Viwango vya ubora.