Dar es Salaam. Dini zote zinakubaliana kuwa ndoa ni baraka na ni moja ya karama tatu kuu za maisha ya mwanadamu hapa duniani. Karama ya kwanza ni kuzaliwa, ya pili ni ndoa na ya tatu ni kifo.
Na inaelezwa kuwa ndoa hupendeza zaidi pale mtu anapoamua kuingia kwa hiari, akiwa na akili timamu na utayari wa dhati.
Kwa maana hiyo, suala hili haliwezi kufananishwa wala kufungwa na kanuni fulani kama linavyoweza kutafsiriwa na jamii, wazazi, au hata waliotutangulia kama ndugu zetu wa karibu, dada na kaka.
Kumekuwa na kamusi dunia ambayo wengi huiishi na kuifanya kuiabudu kama kanuni, baadhi ya mistari kwenye kamusi hiyo inasema, kabla ya kufikisha miaka 30, basi wazazi waanze kudai mkwe, yaani unaoa lini au unaolewa lini.
Mistari hiyo inawafanya vijana wa kike na wa kiume wapunguze ukaribu wa kuzungumza na wazazi wao na hata ndugu ili kukwepa kuulizwa lini ataingia kwenye taasisi ya ndoa.
Tunapoelekea kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, mara nyingi wanafamilia hukutana pamoja, na swali hili kwa vijana wao huuliziwa sana, hususan kwa waliofikisha umri wa kuoa au kuolewa.
Wazazi wengi wanapouliza swali la “unaoa au unaolewa lini”, mara nyingi hufanya hivyo kwa nia njema ya kutaka kuhimiza watoto wao kuingia kwenye hatua muhimu ya maisha.
Hata hivyo, swali hili linaweza kuwa na athari tofauti kwa vijana wanaolengwa, kwa sababu mara nyingi hujenga presha na kuleta hisia za kero.
Swali hili linapokuwa la mara kwa mara, vijana huanza kulichukulia kama kero, hali inayoweza kuwasababisha kuanza kuwakwepa wazazi wao kwa njia mbalimbali.
Baadhi huacha kupokea simu, kujitenga na familia au hata kuepuka kwenda nyumbani wakati wa likizo ili tu wasikumbane nalo.
Ingawa nia ya wazazi inaweza kuwa njema, uamuzi wa kuingia kwenye ndoa si jambo rahisi. Linahitaji mtu kuwa na utayari wa kiakili, kihisia, na kiuchumi.
Ni muhimu kwa wazazi kujiuliza je, kijana wao yuko tayari kwa majukumu mazito ya kifamilia kama baba au mama?
Ritha Peter, binti mwenye umri wa miaka 25, anasimulia jinsi wazazi wake walivyomfanya hadi akahisi kuwa na presha kutokana na swali hilo.
“Tuna watoto watatu katika familia yetu. Baada ya kaka yangu mkubwa kuoa, swali la ndoa lilianza kunielemea mimi na kaka yangu wa pili. Imekuwa ajenda ya kila kikao cha familia,” anasema Ritha na kuongeza kuwa imeathiri ukaribu na wazazi wake.
“Nikiwa mbali na nyumbani, nikiiona simu ya baba au mama naingiwa na hofu kwa sababu najua ataniuliza swali hilo.
Lakini anakiri kuwa wakati mwingine hufikiria kuingia tu kwenye ndoa bila kujali, lakini hutafakari zaidi na kugundua kuwa ndoa inahitaji upendo, utayari na mtu sahihi.
“Kujinyima uhuru na furaha kwa kuishi na mtu usiyempenda ni kujinyanyasa,” anasema Ritha.
Hali kama hiyo inamkumba pia Carlos Swai (29) wa Mbuyuni, Dar es Salaam ambaye anasema presha ya familia kuhusu ndoa imekuwa changamoto kubwa kwake. Carlos, kama Ritha, anahisi swali hili linapunguza furaha na ukaribu wake kwa familia yake.
Hata hivyo, anasema ni vema kwa wazazi kuelewa kwamba swali hili linahitaji busara na uvumilivu. Badala ya kushinikiza, wanapaswa kuwapa vijana wao muda wa kujiandaa na kufanya uamuzi wa busara kuhusu maisha yao ya baadaye.
Anasema mazungumzo yenye kujenga na yenye kuzingatia hisia za kijana yanaweza kuimarisha uhusiano wa kifamilia badala ya kuvuruga.
“Binafsi swali hilo silipendi na suala la kuoa linanihusu mimi binafsi na si mtu mwingine yeyote, mimi ndiyo ninafahamu ni wakati gani sahihi kwangu wa kuingia kwenye ndoa, kuna baadhi ya ndugu na wazazi huuliza swali hilo ili kukupima kama una malengo au huna,” anasema.
Anasema kuoa ni malengo, lakini haimaanishi kuwa ni malengo anayopaswa kuanza nayo kwa kuwa maisha hayana kanuni na unaweza kuwahi kuoa ukajikuta maisha yanakuwa magumu zaidi kama ulivyo tegemea.
“Maisha hayana kanuni, inategemea tu Mungu kakupangia nini, suala hili kwa upande wangu halijawahi kunitenganisha na ndugu, ila ni swali ambalo siliendekezi na ninapoulizwa huwa badilisha mada bila kuchangia lolote kuhusu kuoa na nikiona haelewi ananichimba sana huwa nanyanyuka naondoka, kama ni simu, basi naikata,” anasema Carlos.
Sambamba na hilo, mwanasaikolojia Neema Mwankina amesema maswali ya kuoa na kuolewa lini, mara nyingi huwa yanawaathiri vijana wengi kwa namna yanavyoulizwa.
“Kulingana na kasi ya dunia, tabia mbalimbali huibuka kwenye jamii, kama mzazi si vibaya kumuuliza mtoto ataolewa lini, mzazi anapaswa kutafuta njia rafiki ya kuuliza swali hilo bila kumfanya mtoto ajisikie vibaya,” anasema mtaalamu huyo.
Anasema moja ya kosa kubwa wanalolifanya wazazi ni kumuuliza kijana wao mbele za watu au kumshtaki kwa watu kuhusiana na kuoa.
“Kumuuliza mtoto maswali kama hayo mbele za watu ni kumuaibisha, yeye ndiye anafahamu wakati sahihi na aina ya maisha anayotaka kuyaishi, mtoto anapokuwa hajajiandaa kuingia kwenye ndoa kumuuliza au kumshtaki hakusaidii,” anasema.
Mwankina anasema watoto huanza kujitenga na jamii pamoja na wazazi wakihofia maswali hayo, lakini pia hupunguza upendo kwa ndugu na kila anayemuuliza swali hilo.
“Kuna wakati utafika, mtoto atashindwa kushiriki vikao vya kifamilia na kutoa udhuru kila wakati kwa kuhofia kuulizwa maswali kama hayo mbele za watu,” anasema.
Mwankina anasema ni vema wazazi wawe na upendo wanapowauliza vijana wao swali hilo, ili mtoto awe muwazi na pengine amuombe ushauri kama kuna gumu anapitia na hajui nini afanye.
Aidha, baadhi ya viongozi wa dini wameweza kutoa maoni yao kuhusu namna kijana anavyoathiriwa na maswali ya kuoa na kuolewa lini katika mfumo mzima wa kutafuta mwenza wa maisha.
Aliyekuwa Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini anasema kumuuliza kijana unaoa lini kila wakati inampa presha katika kutafuta mwenza wa maisha.
“Kijana anapaswa kupewa muda wa kutosha na fursa ya kutafuta mwenza sahihi, unapouliza kila wakati unaharibu afya ya kijana kiujumla,” anasema Askofu Kilaini.
Anasema kauli hiyo upande wa mtoto wa kike humharibia zaidi tofauti na mtoto wa kiume na pia huweza kumletea madhara.
“Mara nyingi msichana anapoulizwa kila wakati anakosa utulivu wa nafsi na kuanza kusaka mume kwa namna yoyote ile, huku wengine wakibeba ujauzito na kuhisi ni njia ya kujipatia mume kirahisi, lakini baadaye huishia kutelekezwa na kulea watoto wenyewe,” anasema.
Askofu Kilaini anasema kama kiongozi wa dini anakutana na visa vingi na migogoro ya wanandoa na nyingine huvunjika kabisa na sababu kuu ni kukosekana kwa upendo kati yao.
“Ndoa nyingi zinakumbwa na migogoro, ila ukikaa chini na kuwasikiliza, utagundua hawakuwa na muda wa kutosha kuchunguzana katika uchumba na ukiuliza zaidi jibu linakuja walioana ili kuwaridhisha wazazi baada ya kuulizwa swali hilo kwa muda mrefu,” anasema Askofu Kilaini.
Sambamba na kiongozi huyo wa dini, Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema hivi sasa kuna migogoro mingi ya ndoa changa na sababu ni wenza kutoridhiana wakati wa kufunga ndoa.
“Kuna migogoro mingi ya ndoa changa kutokana na watoto kulazimishwa kuingia kwenye ndoa baada ya wazazi kuona hakuna dalili za wao kutaka kuingia kwenye taasisi ya ndoa,” anasema Kitogo.
Hata hivyo, anasema misingi ya ndoa za kidini ni mtu kufikia muda wa kuoa na kuolewa, japokuwa misingi hiyo inamtaka mtu binafsi kuwa tayari.
“Kidini, umri sahihi wa kijana kuoa ni ule muda wa kuwa na uwezo wa kumtunza mke wake katika maisha yao yote na katika uhalali unaotakiwa,” anasema.
Na anasema katika sura mbalimbali kwenye kitabu cha dini, inasisitiza kijana kuoa mke anayemtaka na kuolewa na mume anayemtaka bila kulazimishwa na mtu yeyote.
“Mzazi unapomhoji kijana kila wakati inapelekea akimbilie kuoa mtu bila kumridhia, mara nyingi watu hawa hukosa uvumilivu inapotokea sintofahamu katika ndoa kwa sababu ya kuishi kwa mapenzi ya kupandikizwa na siyo hiari binafsi,” anasema.
Sheikh Kitoga anatumia nafasi hiyo kuwaasa wazazi wa pande zote kuwa walezi wa ndoa za watoto wao ili ziweze kudumu muda mrefu pasipo kupeana talaka.
“Kingine wazazi waanze kutoa mafunzo kwa watoto wao pale wanapofikia umri wa utu uzima, hii itasaidia mtoto kukua akijua kuna maisha ya ndoa baadaye, mafunzo haya yatasaidia kumjenga mtoto tofauti na kumpa presha pale anapofikia umri sahihi wa kuoa na kuolewa,” anasema.