Dar es Salaam. Kalenda ya mwaka wa masomo kwa 2024 imehitimishwa Desemba 6. Kuhitimishwa kwa kalenda ni ishara ya kuanza kwa msimu wa likizo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini itakayodumu kwa takribani siku 30.
Likizo ni wakati wa kupumzika, kufurahi, na kujifunza mambo mapya, lakini pia ni wakati mzuri wa kuboresha uhusiano na familia na kujenga tabia nzuri.
Hiki ni kipindi kizuri cha kujenga uhusiano wa karibu na familia, kwa kuwa inatoa fursa kwa watoto kujumuika pamoja katika shughuli za familia, kama vile kupika pamoja, kusafiri, au kufanya kazi za nyumbani, wanajenga uhusiano mzuri na pia wanafundishwa umuhimu wa kushirikiana na kusaidiana.
Hii ni nafasi nzuri ya kuwafundisha watoto maadili ya familia na kuwajenga kimaadili kama ambavyo mara kadhaa Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahaba amekuwa akisisitiza.
Kiongozi huyu amekuwa akitoa msisitizo kwa wazazi kutumia kipindi cha likizo kuwafundisha watoto kazi za mikono kulingana na umri wa mtoto husika na uhusiano wa kijamii.
Anasema likizo si kwa sababu ya wanafunzi kupumzika pekee, bali ni fursa pia ya watoto kujifunza vitu vingine, ikiwemo kazi na kuchangamana na wanajamii.
“Usidhani hali nzuri uliyonayo leo itadumu milele, maisha hayatabiriki, leo upo hivi kesho utakuwa vile, kwa hiyo mpe mtoto wako maarifa, maadili na elimu ya mikono. Muache mtoto afanye kazi, alime, afagie banda, adeki, achimbe shimo la takataka, maisha ni maarifa hivyo mpe maarifa, mpe maadili, mpe na ujuzi”.
“Tunaposema watoto wapumzike wakati wa likizo tuna maana kwamba anatakiwa kupumzisha akili kujifunza masomo ya darasani na kutumia nafasi hiyo kujifunza vitu vipya,” anasema na kuongeza:
“Mfundishe mtoto vitu vingine, ikiwemo kazi za mikono, shughuli mbalimbali za kijamii kulingana na umri wa mtoto. Ni kipindi ambacho mtoto anaweza kuwekwa karibu na ndugu na jamaa, kama atakuwa shule Januari hadi Desemba atawajua lini ndugu, atajifunza lini kuhusu utamaduni wake.”
Mbali na kamishna huyo, watu mbalimbali waliozungumza na Mwananchi wameshauri wazazi kutumia kipindi hiki cha likizo kuhakikisha watoto wao wanajifunza vitu vingine nje ya masomo.
Leah Mwangosi, ambaye kitaaluma ni mwalimu anasema ujifunzaji wa kazi za nyumbani ni eneo lingine linalopaswa kupewa kipaumbele katika kipindi hiki cha likizo.
Leah anasema vijana wengi wa sasa hawamudu kufanya kazi za nyumbani kwa kisingizio cha masomo, hivyo kipindi ambacho wapo likizo ni muhimu wazazi kuhakikisha wanawafundisha watoto wao umuhimu wa kujua jinsi ya kufanya kazi hizo.
“Kwa umri wa mtoto wa sekondari ni kawaida kabisa kuachiwa nyumba na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, lakini hawa watoto wetu wa siku hizi hawajiwezi, unakuta binti hadi anamaliza kidato cha nne hawezi kupika wala kufua nguo ikatakata. Ikitokea umepata safari ya ghafla na umemuacha basi njia nzima utakuwa unawaza kinachoendelea nyumbani.
“Hao watoto wa kiume nao ni changamoto, unaishi na kijana wa miaka 17 hadi 18 ndani halafu unaenda kutafuta fundi wa kuweka balbu au kukata majani kwa sababu mtoto wako hawezi kufanya hizo kazi. Hatupaswi kuwalea watoto kwa mtindo huu, ni kweli elimu ni muhimu, ila wanapaswa pia kujifunza kazi za nyumbani na kipindi hiki cha likizo ndio wakati sahihi wajifunze na wafanye hizo kazi,” anasema Leah.
Mdau wa elimu, Ochola Wayoga anaweka msisitizo kuwa katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wanakuwa katika likizo ya mwaka na wale waliohitimu kidato cha nne wanasubiri matokeo, ni muhimu kuhakikisha wanapata shughuli za kufanya katika mazingira yanayowazunguka.
Anasema hatua hiyo itawafanya kujifunza kufanya kazi za mikono, hasa za uzalishaji mali, akitolea mfano kilimo cha bustani ya mbogamboga, ufugaji na shughuli nyingine ambazo zinafanyika nyumbani au katika mazingira ya karibu na anapoishi.
Mbali na hilo, Wayoga pia ametaka wazazi wa wahitimu wa kidato cha nne kutumia kipindi hiki kuhakikisha vijana wao wanashiriki kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii yao ili kuwatengeneza kuwa raia wanaojitambua na kujitoa kwa ajili ya jamii.
“Mtoto aliyemaliza kidato cha nne anaelekea kwenye kundi la vijana, hivyo ni muhimu wajifunze kushirikiana na wanajamii kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, iwe mjini au kijijini, hii maana ya elimu na kujifunza ushiriki wao kwenye shughuli za kijamii, ni lazima wafundishwe kuwajibika. Siyo muda wote kwenye TV, simu.
“Wenye uwezo wa kujitolea hata kufundisha kwenye shule za msingi waombe kwa kufuata taratibu katika shule husika na endapo watapata fursa hiyo wafanye kwa uaminifu. Zipo shule nyingi huko pembezoni zina changamoto ya walimu, sasa wakiwepo vijana hawa ambao watathibitika kuwa wana uwezo wa kufundisha si vibaya wakafanya hivyo,” anasema Wayoga.
Mbali na hilo, anashauri wazazi wawafundishe vijana hawa mbinu za kujiwezesha kiuchumi na ikiwezekana wawape nafasi ya kujionea wanachokifanya kwenye shughuli zao zinazowaingizia kipato.
“Kama wazazi ni wakulima wasisite kwenda na kijana huyu shambani, hivyo hivyo kwa mzazi mfanyabiashara nenda naye kwenye eneo lako la biashara, muonyeshe nini unafanya na unafanyaje, hii itampa fursa ya kuona na kujifunza kinachofanyika kwenye shughuli husika ya uzalishaji, unaweza pia kumpeleka kwa mtu ambaye anafanya shughuli za aina hiyo ili aweze kujifunza na sio kukaa nyumbani bila shughuli yoyote ya kufanya,” anasema Wayoga.
Kwa upande wake mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Richard Hananja anasema wakati wa likizo ni fursa nzuri kwa watoto kujivunia, kujifunza na kukua kimaadili.
Anasema wazazi ndio wenye jukumu la kutoa majibu ya maswali yanayoikumba familia, kwa kufanya hivyo wanajijengea heshima na thamani.
Anasema ni muhimu kwa wazazi kupata muda wa kutosha wa kuwa na watoto ili wawajenge katika mfumo unaofaa, kinyume na hapo atakutana na watu wengine nje watakaowapandikiza yasiyofaa.
Mchungaji Hananja anaeleza: “Sauti ya wazazi katika malezi na makuzi ya watoto ni muhimu, mzazi una nafasi ya kumjenga mtoto wako vile unataka, mtengenezee mwelekeo wa maisha. Mtoto kuanzia mwaka 0 hadi miaka 14, ndio umri wa kumtengeneza, sasa kama huna muda wa kukaa naye ukapandikiza vitu vizuri ndani yake tegemea watu wengine kufanya hivyo”.
Leticia Mbando, ambaye ni mzazi anasema ili kukabiliana na tatizo la mmomonyoko wa madili ni lazima hatua zichukuliwe na zinapaswa kuchukuliwa kuanzia chini na hasa kwenye mfumo wa elimu, kwa kuwa ndiyo watu wote wanapitia.
“Suala la nidhamu halipaswi kuwa la mjadala, ni utekelezaji wake ndio unatakiwa, tunahitaji kizazi chenye nidhamu na kuzingatia maadili, siku hizi si kitu cha ajabu kuona mtoto anamtolea maneno makali mtu mzima au anashindwa hata kumpisha kwenye kiti akae,” anasema Leticia.
Hata hivyo, mama huyu anasema ili kutengeneza watoto wenye maarifa, maadili na ujuzi ni lazima uwepo ushirikiano wa kutosha baina ya wazazi, walimu na jamii kwa jumla.
“Shule zinaweza kuwa msaada mkubwa katika kutengeneza kizazi chenye nidhamu na maadili endapo mkazo utawekwa katika taasisi hizo ambazo zinakaa na watoto kwa muda mrefu kuliko wanavyokuwa nyumbani, wazazi pia tunapaswa kuwajibika katika hili”.
Wakati wa likizo ni wakati mzuri wa kuwafundisha watoto ujuzi wa kujitunza, kama vile kudumisha usafi, kupanga vitu vyao, na kuchukua majukumu nyumbani. Hii itawasaidia kuwa na tabia nzuri na kuwajenga kuwa na nidhamu na uwajibikaji katika maisha yao.
Abdul Jumaa, ambaye ni mtaalamu wa Tehama anasema katika dunia ya leo, teknolojia ni sehemu muhimu ya maisha ya kila mtoto, hivyo wazazi wanaweza kutumia kipindi cha likizo kuhakikisha watoto wao wanajifunza vitu muhimu vya teknolojia.
Anasema: “Wazazi wanaweza kuwaongoza watoto katika kuchagua programu au michezo ya kielimu ambayo itawaongezea maarifa na ujuzi mpya. Hata hivyo, ni muhimu kuweka mipaka ya muda wa kutumia vifaa vya kielektroniki ili kuepuka athari mbaya za matumizi ya muda mrefu”.