Mvua yaua watano Rukwa, yumo mama na mwanawe

Rukwa. Watu watano wamefariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Rukwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Sherdack Masija, ameyasema hayo  Jumamosi Novemba 7,2024 wakati akizungumzia tukio hilo.

Kamanda Masija amesema watu hao wamefariki dunia, kwa nyakati tofauti katika wilaya za Sumbawanga,  Kalambo na Nkasi.

Amewataja marehemu  kuwa ni Maiko Simuni (70), mkazi wa kijiji cha Kalahela Wilaya ya Kalambo ambaye alifariki Novemba 31, 2024 baada ya kutumbukia kwenye shimo lililokuwa limejaa maji.

Mwingine ni Coletha Chaula (74), mkazi wa Kijiji cha Kaoze Wilaya ya Sumbawanga aliyefariki Desemba 3, baada ya kutumbukia kwenye korongo lililokuwa limejaa maji.

Naye, Chausiku Nyampasa (42) mkazi wa Kijiji cha Legeza Mwendo Wilaya ya Kalambo, aliyefariki Desemba 5, akiwa na mtoto wake aliyejulikana kwa jina la Segile  Simfukwe (4) ambao wote walifariki baada ya kusombwa na maji wakivuka mto Masazi.

Kamanda huyo alimtaja mtu wa tano kuwa ni Masunga Kaigi (70), mkazi wa Wilaya ya Nkasi aliyafariki jana, baada ya kuanguka kwenye dimbwi la maji akiwa anatembea barabarani.

“Kwa hiyo wote hawa utaona wamefariki kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwenye mkoa wetu.

“Nitoe wito kwa wananchi katika kipindi hiki kuepuka kuruka mito ili kuepusha vifo vinavyoweza kuepukika, kwa kuwa sehemu ambazo hazikuwa na maji hivi sasa zina maji,” amesema Kamanda Masija.

Pia, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), hasa wanaoenda  ziwani kwa ajili ya shughuli za uvuvi na usafiri.

Related Posts