YANGA imemshusha kocha wa mazoezi ya viungo mpya, Adnan Behlulovic ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka mzozo kati ya kocha mkuu wa timu hiyo, Sead Ramovic na kocha wa mazoezi hayo aliyemkuta Taibi Lagrouni.
Kupishana kwa wawili hao, kisha Lagrouni kukacha safari ya kwenda na timu hiyo Algeria, imefanya mabosi wa Yanga haraka kuingia kazini kwa kufuata matakwa ya Ramovic na kumsafirisha Behlulovic moja kwa moja akitokea Ujerumani hadi Algeria kisha kuanza kazi juzi usiku wakati kikosi cha mabingwa hao wa soka Tanzania kikifanya mazoezi ya mwisho kabla ya jana kucheza dhidi ya wenyeji wao MC Alger.
Behlulovic aliyezaliwa miaka 43 iliyopita mara baada ya kutua na kujiunga na timu hiyo, aliwasoma wachezaji wa kikosi hicho na akawapa taarifa ya awali mabosi wa timu hiyo kwamba ufiti wa mastaa uko chini kulingana na falsafa ya Ramovic, lakini akawashusha pumzi kwamba ndani ya wiki chache kila kitu kitakuwa sawa.
Kocha huyo ambaye ni raia wa Bosnia-Herzegovina amewaambia mabosi wa Yanga mara baada ya timu hiyo kurejea nchini kazi ya kupandisha utimamu wao wa mwili itaanza haraka kwa vipindi tofauti kwa kuwa bado kikosi hicho kipo kwenye ratiba ngumu ya mechi za mashindano.
“Kocha amesema kuna wachezaji ambao wako fiti na wengine wako katikati na kuna wale ambao wako chini kidogo, ameomba wiki chache kufanikisha kuwaweka kwenye daraja moja la utimamu wa mwili,” alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga aliyeambatana na timu hiyo Algeria.
Hata hivyo, ingawa Yanga imetoa taarifa Behlulovic atakuwa akifanya kazi pamoja na Lagrouni, ila taarifa za ndani Mwanaspoti inazo ni Lagrouni atashushwa kwanza timu ya vijana kwa muda na huenda baadaye akaondoshwa.
Maamuzi ya kutakiwa kuondoshwa kwa Lagrouni ni kuweka maelewano sawa na benchi la Ramovic ambaye ndiye aliyetofautiana kwa maneno na kocha huyo raia wa Morocco aliyekuja wakati wa kocha aliyesitishiwa mkataba Miguel Gamondi.
Ramovic alitofautiana na Lagrouni juu ya utimamu wa mwili wa wachezaji wa timu hiyo na Mjetumani huyo alitaka kuona inafanyika kazi ya kuwapandisha juu ya ubora huo, huku Mmorocco huyo akigoma akidai kitakachofanyika kipo nje ya taaluma yake.
“Kwa sasa Lagrouni atabaki, lakini baadaye sidhani kama ataendelea kuwa sehemu ya benchi la Ramovic kwa kuwa wameshaonyesha kutoelewana mapema tena kila mtu akisimamia taaluma yake, hii ni hatari kwa afya ya benchi la ufundi,” alisema mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga. Endapo Lagrouni ataondoka hii itamaanisha atabaki kocha mmoja pekee ambaye alikuja mapema wakati wa ujio wa Gamondi, akisalia kocha wa makipa Alaa Meskini ambaye naye ni raia wa Morocco.