Geita. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, imebariki kutiwa hatiani na adhabu ya kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa aliyekuwa askari wa Jeshi la Polisi mwenye cheo cha Koplo, Mathew Lusangija.
Ushahidi uliomtia hatiani unaonyesha Lusangija alimfuata Burugu Malingila, na kumtuhumu kuhifadhi wahamiaji haramu na kujihusisha na uganga wa jadi bila kibali, na kumtaka ampe Sh1 milioni ili asimfungulie mashtaka ya jinai.
Aprili 14, 2023 Malingila ambaye ni mkazi wa kijiji Bulangale, Wilaya ya Nyang’hwale aliomba apunguziwe kiasi hicho hadi Sh800,000 licha ya kuwa tuhuma hizo zilikuwa ni za uongo na alihofu kubambikiwa kesi hiyo.
Katika utetezi wake, Lusangija alikiri kuwa siku ya tukio alikuwa katika kijiji cha Bulangale kwa ajili ya kuchunguza kifo cha mashaka cha mtoto na kwamba Malingila ndiye aliyedaiwa kuutakasa mwili wa marehemu huyo.
Wakati akijitetea ili kujinasua na shtaka hilo, ‘polisi’ huyo alikanusha madai ya kupokea hongo hiyo na kudai alishushiwa tuhuma hizo kama sehemu ya mpango wa awali wa kuzuia uchunguzi wake kuhusu kifo cha mtoto huyo.
Kutokana na ushahidi uliotolewa dhidi ya ofisa huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi, Mahakama ya Wilaya ya Nyang’hwale ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh500,000 au kifungo cha miaka mitatu, akakata rufaa kupinga hukumu.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza sababu zake tatu za rufaa, Jaji Graffin Mwakapeje katika hukumu yake aliyoitoa Desemba 6, 2024 aliitupa rufaa hiyo na kubariki kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa na mahakama kuwa ilistahili.
Ushahidi uliomtia hatiani
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri ambaye ni ofisa mchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Stanley Wambura alidai anakumbuka namna Malingila alivyomtuhumu mrufani kudai rushwa hiyo.
Mrufani inaelezwa alimpa wito mwananchi huyo kufika ofisi za mtendaji wa kijiji cha Bulangale na kumpa tuhuma za uongo kuwa anajihusisha kuhifadhi wahamiaji haramu na kumtaka atoe rushwa ya Sh1 milioni lakini akatoa Sh800,000.
Malingila aliyekuwa shahidi wa pili wa Jamhuri, alieleza kuwa Aprili 14, 2023 aliitwa ofisi za mtendaji wa kijiji ili kukutana na ofisa huyo wa Polisi.
Katika ofisi hizo, ofisa huyo akiwa na mgambo alimtuhumu kuhifadhi wahamiaji haramu na uganga wa jadi bila kibali na alitaka apewe fedha hizo ili asimfungulie mashitaka, ikabidi aende kukopa fedha hizo kutoka kwa Richard Mhena.
Wakati akirudi katika ofisi za mtendaji huyo wa kijiji, mrufani alisimamisha pikipiki waliyokuwa wamepanda na kutaka apewe fedha hizo hapo hapo na mabadilishano hayo ya fedha yalishuhudiwa na mashahidi wengine watatu.
Ushahidi wa mashahidi wengine ulikuwa hautofautiani na uliotolewa na ofisa mchunguzi kutoka Takukuru na mlalamikaji mwenyewe na kwamba baada ya mrufani kuchukua fedha hizo, mlalamikaji alitoa taarifa Takukuru.
Katika hukumu yake, Jaji Mwakapeje alichambua hoja zote tatu za rufaa ambazo ni pamoja na kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo, hakimu alikosea kuchambua ushahidi na alishindwa kuzingatia ushahidi wa utetezi wake.
Jaji alisema madai ya mrufani kuwa tuhuma za rushwa dhidi yake ni katika kutaka kuzuia uchunguzi wa kifo cha mtoto, unakosa ushahidi wa kuunga mkono.
“Kumwita shahidi wa pili (mlalamikaji) na kuendelea kumshinikiza atoe pesa licha ya kutokuwepo kwa ushahidi unamhusisha na tuhuma alizopewa ilikuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka,”alisema Jaji Mwakapeje na kuongeza:
“Madai ya mrufani kuwa tuhuma za rushwa zilikuwa ni za kutengeneza haishawishi kwa kuwa haiungwi mkono na ushahidi na inaonekana ni katika kutaka kujinasua.”
Kuhusu kama upande wa Jamhuri ulithibitisha kosa hilo pasipo kuacha mashaka, Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa pili na wa tatu ulijenga msingi kuwa mrufani aliomba na kujipatia fedha kutoka kwa shahidi wa pili aliyekuwa mwathirika.
“Ushahidi wa shahidi wa nne na wa tano unathibitisha kuwa kuna fedha ambazo mlalamikaji alikopeshwa na alikabidhiwa mrufani njiani na haukubishaniwa. Ushahidi wa shahidi wa saba nao unaonyesha kulikuwa na jambo liliendelea.”
Jaji alisema utetezi alioutoa mrufani haukuweza kutikisa uzito wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na unathibitisha alichukua fedha kutoka kwa mlalamikaji akihofia kubambikiwa makosa na mrufani huyo.
“Nimeridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mashitaka pasipo kuacha mashaka na utetezi wa mrufani hauna mashiko. Kwa hiyo nathibitisha kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa. Rufaa yako inatupwa,”alisema Jaji.