Hivi ndivyo unavyoweza kujinasua dhidi ya uraibu wa ‘kubeti’

Dar es Salaam. Kama unashiriki michezo ya bahati nasibu ‘kubeti’ na umefikia hatua unatamani kuacha na unashindwa, zipo mbinu kadhaa zitakazokusaidia kufanikisha hilo.

Kwa mujibu wa ushuhuda wa waliofanikiwa kujinasua kutoka kwenye uraibu wa kubeti, si rahisi kujitenga na michezo hiyo, ingawa inawezekana.

Sambamba na ushuhuda wa waraibu, wanazuoni nao wanaunga mkono uwezekano wa kuondokana na uraibu huo, wakisisitiza kujenga tabia mpya ni moja ya mambo muhimu.

Mkazi wa Dar es Salaam, Selemani Baini anasema alijinasua kutoka kwenye uraibu huo kwanza kwa kujijua na kukubali ameathirika na kamari.

Anasema wengi hawawezi kuona madhara ya kamari kwa sababu ni jambo linalojificha chini ya ndoto za kushinda.

Hata hivyo, anasema wakati mmoja au mwingine, mtu anayekumbwa na tatizo la kamari anagundua haathiriki kifedha pekee, bali pia afya yake ya akili, uhusiano wa kifamilia na ustawi  wa kijamii.

“Nikawa natathmini hali yangu na kuwa mkweli kwa kujulisha wengine kuhusu matatizo ninayoyapata kutokana na kamari.”

“Ukweli ni aibu, lakini kujitambua na kukubali kwamba kuna tatizo ni hatua muhimu,” anasema.

Mbali na Baini, Degela Michael anasema alijitenga na kubeti baada ya kutafuta na hatimaye kupata msaada.

Anasema kwa uzoefu wake, amebaini kamari ni ugonjwa unaohitaji matibabu ya kiakili, msaada wa kisaikolojia na kutoka kwa familia, marafiki na makundi ya kijamii.

Kwa mujibu wa Michael, alitumia wataalamu wa saikolojia wanaotoa msaada wa akili ili kujitenga na michezo hiyo.

Kujenga ratiba, tabia mpya

Ushuhuda mwingine ni kutoka kwa Demona Masika anayesema kuachana na kamari kunahitaji mabadiliko katika mtindo wa maisha.

Ili kufanya hivyo, anasema ni muhimu kuunda ratiba ya kila siku inayoshughulikia kazi, masomo, familia na burudani bila kujumuisha kamari.

“Hii inajumuisha kupunguza wasiwasi kwa kutumia muda wako kwa shughuli nyingine zinazokupa furaha na mafanikio,” anasema akieleza ndiyo siri ya mafanikio yake.

Katika ratiba hiyo, anasema inahitaji kujenga tabia za afya kama kufanya mazoezi au kushiriki katika shughuli za kijamii ambazo zinafaa.

“Kwa kujenga ratiba hii, mtu anaweza kujiepusha na vishawishi vya kamari, kama vile kwenda kwenye kasino, kucheza kamari kwenye mtandao au kushiriki kwenye mashindano ya michezo ya kubahatisha,” anasema.

Kuepuka mazingira ya kamari

Hata hivyo, anasema mazingira ni mfumo muhimu wa ushawishi kwenye uraibu wa michezo hiyo.

Anasema alijikuta akicheza kamari kwa sababu ya mazingira yanayomzunguka.

“Ili kuachana na kamari, mtu anahitaji kuepuka kabisa mazingira hayo,” anasema.

Anasema watu wanaoshiriki kamari mara nyingi huwa na shida katika kuweka malengo ya maisha.

Anasema ni muhimu kujenga malengo madhubuti ya kifedha, kijamii na ya kiafya.

“Malengo haya yanaweza kujumuisha kuepuka matumizi yasiyo ya lazima (kama kamari), kuokoa fedha, kupata kazi au kufanya kazi ya kujitolea,” anasema.

Anasema kuweka malengo yanayohusiana na maisha bora ni moja ya njia za kujenga mtindo wa maisha usio na kamari.

Anasema alijinasua kutoka kwenye kamari baada ya kupata msaada wa kijamii.

“Watu wengi wanaoshiriki kamari wanapitia hali ya kutengwa kijamii na kihisia, na mara nyingi hujikuta wakikosa ushirikiano na familia, marafiki na jamii zao,” anasema.

Kukubali mipango ya kupona

Mchakato wa kuachana na kamari anasema hauendi kwa kasi na mara nyingi kuna matukio ya kushindwa au kurudi nyuma.

“Hii ni sehemu ya mchakato wa mabadiliko, na ni muhimu kujua  kushindwa si kumaanisha kumaliza safari ya kupona,” anasema.

Badala yake, anasema kujifunza kutokana na makosa na kuendelea mbele ni njia bora zaidi.

Anasema kuendelea mbele na kujijengea subira ni muhimu kwani mabadiliko ya tabia huchukua muda na jitihada nyingi.

Dk Anna Gosbert, ambaye ni mtaalamu wa saikolojia, anasisitiza kujitambua na kukubali tatizo, husaidia mtu kuwa na nguvu ya kutafuta msaada na kufanya mabadiliko katika maisha yake.

Anatoa wito kwa watu kuondokana na aibu na kuona kwamba mabadiliko yanawezekana iwapo watajitahidi kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nia thabiti ya kuachana na uraibu.

Mshauri wa masuala ya kifedha, James Mwenje anasema kamari inahusiana na matumizi mabaya ya fedha.

“Watu wengi wanatumia fedha kwenye kamari kwa sababu ya kutojua namna ya kusimamia fedha zao,” anasema.

Mtaalamu wa afya ya akili, Dk Athony Mwita, anaeleza kamari ni ugonjwa wa akili na inahitaji matibabu ya kitaalamu.

“Kamari ni ugonjwa wa akili na tiba ya kiakili kama vile Cognitive Behavioral Therapy (CBT) inaweza kusaidia kubadilisha mitindo ya mawazo na tabia za kamari,” anasema.

Aidha, anatoa wito kwa jamii kutambua umuhimu wa kutoa msaada kwa watu waliothirika na kamari, badala ya kuwahukumu.

“Kumsaidia mtu aliyeathirika na kamari kunahitaji uelewa, sio hukumu,” anasema Dk Mwita.

Kwa upande wake, Mshauri wa masuala ya kijamii,  Emmanuel Kizito anasema kujenga ratiba na tabia mpya ni hatua muhimu katika mchakato wa kuachana na kamari.

“Unapokuwa na ratiba inayojumuisha kazi, masomo, na shughuli za kijamii, inakuwa rahisi kuepuka vishawishi vya kamari,” anasema.

Related Posts