Ambundo ashtukia jambo Ligi Kuu Bara

WINGA wa Fountain Gate, Dickson Ambundo ameiangalia Ligi Kuu Bara na kubaini msimu huu kumekuwa na ushindani mkubwa, wakati hata haijamaliza duru la kwanza, huku akisisitiza ushindani huo umetoa funzo kubwa kwake akiamini anapaswa kukaza buti ili ngwe pili timu yao ifikishe malengo.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na Dodoma Jiji, anayemiliki mabao mawili alisema jambo la msingi ni kutanguliza masilahi ya timu kufanya vizuri ndipo ya kwake yafuate.

“Timu ina malengo yake ndiyo maana ikaona umuhimu kunisajili, hilo siyo kwangu pekee, bali kwa kila mchezaji, timu ikifanya vizuri ni rahisi mchezaji kuonyesha kiwango cha juu,” alisema Ambundo na kuongeza;

“Timu zimesajili vizuri ndio maana kuna ushindani mkali, binafsi najipanga zaidi nikijua mzunguko wa pili hautakuwa wa mchezo, binafsi natamani tumalize msimu ndani ya nafasi tano za juu.”

Mbali na hilo, alimtaja beki bora kwake katika Ligi Kuu ni Dickson Job wa Yanga, alimuelezea ni mtulivu wa kuondoa mashambulizi golini na ana uwezo wa kuzungumza na wachezaji wenzake pindi wanapokuwa wanajihasau kutimiza majukumu yao.

“Kwanza ni kiongozi mzuri dhidi ya wengine, mtulivu wa kuokoa hatari zinazokuwa zinaelekezwa golini kwao, jambo linalosaidia kutofanya makosa ya kuigharimu timu,” alisema.

Fountain Gate kwa sasa ipo nafasi ya saba ikicheza mechi 12 na kushinda tano, ikitoka sare mbili na kupoteza tano.

Imefunga mabao 30 na kufungwa 21 ikimiliki pointi 17, huku nyota wake wawili Seleman Mwalimu mwenye mabao sita na Edger William mwenye matano wakichuana na mastaa wa timu nyingine katika orodha ya wafungaji wa ligi hiyo itakayoendelea tena Desemba 11 baada ya kusimama kupisha michezo ya Kombe la Shirikisho hatua ya 64 Bora.

Related Posts